LIGI Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili, Ligi ya Wanawake pamoja na masuala yote yanayohusu michezo yamesimamishwa kwa muda wa mwezi mmoja.
Chanzo kikubwa kilichofanya haya yatokee ni maambukizi ya Virusi vya Corona ambavyo ni janga la dunia kiujumla.
Familia ya michezo imekuwa kwenye huzuni na inaungana na dunia nzima kuendelea kuchukua tahadhari ya kupambana na Virusi hivi ambavyo kasi yake inazidi kuwa kubwa.
Tunaona kwamba dunia nzima imeungana na inapambana kutafuta suluhisho la tatizo hili ambalo imani yetu ni kwamba Mungu atatenda mema na litapita kama mengine yalivyopita.
Kwa wanamichezo tunaona kwamba hakuna kinachoendelea kwenye michezo hata kwetu Bongo wachezaji wamepewa mapumziko kwa muda kabla ya ligi kuendelea.
Mapumziko haya itakuwa vizuri kwa kila mmoja kuyatumia vizuri kwa manufaa yake pamoja na timu badala ya kuyatumia vibaya kwa kuendela na ratiba ambazo zipo nje ya malengo ya timu.
Kwa wakati huu ambao timu zote zipo kwenye mapumziko ni muhimu kila mchezaji kukumbuka yale aliyopewa wakati wakiondoka kambini na kuelekea kwenye mapumziko hayo.
Kipindi hiki nina amini wachezaji wamepewa programu maalumu na makocha wao ili wakaendelee kulinda viwango vyao hilo ni la msingi kulizingatia ili kupata matokeo chanya.
Wachezaji wajitambue kwamba bado wana kazi ya kufanya na timu yao ligi haijaisha ni lazima waendelee kujipanga na kufanya mazoezi ili wabaki kwenye ubora wao.
Thamani ya mchezaji ni kuwa ndani ya uwanja na kuonyesha uwezo wake muda wote bila kujali kwamba ni wakati gani anahitajika kucheza ni lazima awe tayari kufanya kazi muda wote.
Kazi ya mchezaji ni kucheza tena kwa kiwango bora muda wote awapo uwanjani bila kujali yupo kwenye mazingira gani hivyo jukumu la kulinda kipaji linamhusu mchezaji wwenyewe.
Kwa hali ilivyo kwa sasa mchezaji itakuwa ngumu kujua ligi itaanza lini hivyo endapo atabweteka itakuwa rahisi kwake kuiangusha timu na uwezo wake ambao ndo unaompa ugali.
Endapo wataendelea kufanya mazoezi itawapa nafasi ya wao kutokuwa na hofu ya kurejea kwenye ushindani wa ligi pale ambapo watahitajika kufanya hivyo baada ya muda uliotolewa na Serikali kukamilika.
Itawasaidia kurejea ubora wao wenyewe iwapo watafuata zile program ambazo wamepewa na makocha kwani nina amini kila timu ambayo wachezaji wameondoka kambini hilo ni jambo la kuzingatiwa.
Wakichukulia mapumziko ya sasa kuwa ni likizo itawaumiza kwani watajisahau na kuendelea na masiha yao ya kila siku ilihali ligi bado inawasubiri.
Muda huu kama wachezaji wataamua kula bata watafeli mapema na kuziangusha timu zao kwani bata na mazoezi ni vitu ambavyo havikai kwenye kapu moja kwa wakati huu ambao tunapita.
Ligi inatarajiwa kuendelea na wao wanatakiwa kuendelea kufanya mazoezi ambayo yatawaweka kwenye nafasi nzuri ya kuwa bora muda wote na kufanya kazi yao kwa uaminifu.
Kuna timu ambazo zinapambana kushuka daraja hizi zinapaswa zitambue kwamba wakati huu zikilala ligi itakaporejea itakuwa ni ngumu kwao kupenya kwenye ushindani watakaokutana nao.
Vita ya ubingwa pia inaendelea ambapo kuna timu zinapiga hesabu ya kutwaa ubingwa haitakuwa rahisi kutwaa ubingwa iwapo hakutakuwa na mwendelezo wa mazoezi kwa wakati huu wa mapumziko.
Kubweteka kwao wakiwa nyumbani wanatengeneza mazingira ya kufeli mapema wanatakiwa wasifikirie suala hilo watapata matokeo ambayo yatawashangaza mpaka msimu utakapomeguka.
Itawafanya waanze mwanzo kukiunda kikosi pale watakaporudi ilihali tayari mwendo walikuwa wameshaukamatia kutafuta matokeo ndani ya uwanja.
Jambo lao kubwa ni moja tu kwa wachezaji kuendelea kufanya mazoezi ili wawe bora na kuendelea kuyafukuzia mafanikio ambayo timu inahitaji kuyafikia.
Tahadhari pia ya Virusi vya Corona ni muhimu kwa kila mmoja kuifuata kwani matangazo yanatolewa kila siku namna ya kujikinga na namna bora ya kubaki salama.
Janga ni letu sote halina ambaye hausiki katika wakati huu mgumu ni lazima tukubai kwamba tunapambana kwa pamoja na sio mtu mmoja.
Kila mmoja achukue tahadhari na kujilinda na Virusi vya Corona kila mahali atakapokuwa ni lazima atambue kwamba yeye ni balozi wa mwenzake.
Post a Comment