HUKO mitani na hata kwenye mitandao ya kijamii, mashabiki wa Yanga wamemzulia kitu straika wa Simba, Meddie Kagere baada ya sakata lake na beki Kelvin Yondani, lakini mwenyewe amewasikia na kuwaambia “acheni hizo, ile ni cheni yangu ya dhahabu tu”.

Katika pambano la juzi lililoisha kwa sare ya 2-2, Ally Mtoni ‘Sonso’ aliyekuwa anakabana na Kagere aliiona cheni shingoni mwa straika huyo na kumtonya Yondani ambaye aliikata kijanja kabla ya kukimbilia kwa mwamuzi Jonesia Rukyaa kulalamikia kuvaa kwake cheni hiyo.

Hata hivyo, kulitokea purukushani kidogo na mashabiki kuzua eti ili ‘busta’, lakini Kagere amesema hana mambo hayo ya kipuuzi na kwamba ile ni cheni ya dhahabu na alipitiwa tu kuivua kabla ya kuingia uwanjani, lakini imechukuliwa sivyo ndivyo.

Alisema alikuwa amevaa cheni hiyo kabla ya mchezo kuanza na hata alipokwenda kupasha misuli alikuwa nayo na alijisahau kuivua walipoenda vyumba vya kubadilishia nguo, alisahau kuvua na akaingia nayo uwanjani.

“Nilijikuta nimeingia nayo uwanjani na kuanza kucheza, lakini wakati Yondani ananikaba aliivuta na kuikata, huku akienda kumueleza mwamuzi nacheza nikiwa na cheni jambo ambalo aliichukua na kuipeleka katika benchi letu,” alisema na kuongeza:

“Huwa naivaa muda mwingi kwani hata nikiwa nimelala nakuwa nayo, ndio maana nilijisahau kuivua na nilijikuta nipo nayo uwanjani na muda ambao nilijua kuwa ninayo ni ule Yondani alivyoikata, lakini hakuna kingine cha ziada na mlipoona natafuta kitu ni kidani cha herufi K.”

Naye beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe aliyeshuhudia sakata hilo alisema hakuona kitu chochote tofauti na cheni ya Kagere ambayo Yondani akiwa katika harakati zake za kumkaba aliivuta na kuikata.

“Ni cheni yake ya dhahabu iliyokatwa na Yondani na pale tulipokuwa tunashangaa ilikuwa tunatafuta kidani chenye herufi ya jina lake, lakini tulishindwa kukipata kwa vile mechi ilikuwa ikiendelea,” alisema Kapombe.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.