SASA rasmi kiungo mshambuliaji wa Simba, Hassani Dilunga, amesaini mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kukipiga Msimbazi baada kufikia muafaka mzuri kwa dau la Sh Mil 80.
Kiungo huyo hivi karibuni alikuwa anatajwa kuwepo mipango ya kusajiliwa na Yanga katika kuelekea msimu ujao ambao wamepanga kusuka kikosi chao ili kuhakikisha wanauchukua ubingwa wa ligi na Kombe la FA.
Dilunga amesaini mkataba huo baada ya ule wa awali wa miaka miwili kumalizika mwishoni mwa msimu huu. Alijiunga na Simba kwenye msimu wa 2018/2019 akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa zinaeleza kuwa Dilunga alisaini kwa siri yeye pamoja na kiungo mkabaji Said Ndemla wiki mbili zilizopita baada ya kufi kia muafaka mzuri pande hizo mbili.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Simba hivi sasa bado wanaendelea na mazungumzo na baadhi ya wachezaji wengine waliomaliza mikataba yao ya kuichezea timu hiyo inayonolewa na Mbelgiji, Sven Vandenbroeck.
Aliongeza kuwa Dilunga usajili wake ulipitishwa na kocha Sven ambaye amependekeza abakishwe katika kuiboresha safu ya kiungo ya timu hiyo inayoongozwa na Clatous Chama, Francis Kahata na Sharaff Shiboub.
“Rasmi sasa Dilunga ameongeza mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Simba, hivyo atakuwepo hapa kwa miaka miwili inayofuata ndani ya kikosi chetu cha Simba.
“Dilunga tangu asaini mkataba ana wiki mbili kwani walisaini pamoja siku moja na Ndemla, hivyo hatakwenda popote pale ikiwemo huko Yanga ilipokuwa inaelezwa anakwenda huko.
“Ilikuwa ngumu kumuachia Dilunga kwenda kwingine kutokana na kiwango kikubwa ambacho amekuwa akikionyesha katika msimu huu, amesaini mkataba kutokana na ubora aliouonyesha Simba,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mtendaji Mkuu wa Simba (C.E.O), Senzo Mazingisa hivi karibuni alitamba kuwabakisha wachezaji wote aliowapendekeza kocha ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu huu.
“Hakuna mchezaji yeyote atakayeondoka Simba kwa wale wote ambao tunawahitaji labda wale ambao hatuwahitaji ndiyo watakaoondoka,” alisema Mazingisa.
Chanzo :Championi
Post a Comment