NA SALEH ALLY
JUZI niliandika namna ambavyo wachezaji, viongozi na wadau wengine wa michezo na zaidi nikizungumzia mchezo wa soka wanavyoweza kuitumia vizuri nia ya Rais John Magufuli kutaka kuifungulia michezo.


Nilieleza kuwa wakati Rais Magufuli ameonyesha nia hiyo, litakuwa ni jambo zuri kwa wachezaji, makocha, waamuzi, viongozi na wadau wengine kufanya kile kinachowezekana kuonyesha wanajali na wanachukua tahadhari.
Ninachoamini Ugonjwa wa Covid 19 upo, tuna ushuhuda wa watu wengi, hivyo lazima tuendelee kuchukua tahadhari wakati maisha yetu yanaendelea kurejea kama kawaida, taratibu.


Hatuwezi kukurupuka na ndiyo maana unamsikia Rais Magufuli kuwa kila anapokuwa anazungumza, mwisho anasisitiza suala la kuendelea kuchukua tahadhari.


Kuchukua tahadhari ni muhimu ndio maana nikaeleza namna ambavyo wakati michezo ikiruhusiwa, wadau hao wawe makini na vizuri kuendelea kuchukua tahadhari kusijekuwa na madhara mbele baadaye nia nje ya Rais Magufuli ikaonekana kuwa haikuwa njema.


Jana, Rais Magufuli ametimiza tuliyoiona nia na kuifurahia, kuanzia Juni Mosi sasa ni rasmi kuwa michezo inarejea, sanaa inarejea lakini hata wanafunzi wa kidato cha sita waliokuwa wanajiandaa na mitihani, hali kadhalika vyuo wataingia katika masomo.


Hili ni jambo zuri na inaonyesha namna gani Rais wa nchi yetu anavyotupigania kutokana na nia yake njema kwa sisi na taifa kwa jumla.


Ukipata kiongozi anayepambana kwa ajili yako, ni lazima umuunge mkono lakini vizuri kufanya kazi kwa weledi zaidi ili nia yake njema itekelezeke vizuri.


Hivyo, ushauri wangu mwingine ni kwa wataalamu wanaohusiana na masuala ya afya ambao wanajua kuwa michezo sasa inarejea, wanafunzi wa vyuo wanarejea, kipi sasa cha kufanya.


Kikubwa kabisa ni kuanza kufanya kile ambacho sahihi kwa maana ya wataalamu wa afya kuanza kushirikiana na mashirikisho na vyama vya michezo ili kufanikisha ruhusa hiyo ya Rais Magufuli.


Wataalamu wa afya wao watakuwa wanajua kipi kitakuwa sahihi kufanyika katika wakati huu ambao si wa kawaida kama ule wa zamani.


Ndiyo maana unaona hata katika mazungumzo yake, Rais Magufuli alisema suala la mashabiki uwanjani analiacha kwa Wizara ya Afya.


Anajua kuwa katika wizara hiyo kuna wataalamu na wao wanajua nini cha kufanya kuhusiana na wakati huu kama watu kukusanyika ni sawa au la.


Wakati analiacha suala hilo upande huo, bado Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo itakuwa inawategemea Wizara ya Afya kwa kuwa huku inakuwa ni upande wao na itakuwa sahihi wao ndiyo wawe madereva wa jambo hili.


Utaalamu wa michezo kwa sasa utategemea utaalamu wa afya kwa kuwa tupo katika tatizo la afya katika kipindi hiki tunachojaribu kuendelea kurejea.


Kweli maisha lazima yaendelee lakini lazima kuwe na tahadhari na umakini ili tumpe Rais Magufuli nafasi nyingine ya kuendelea kufungua sehemu nyingine na ikiwezekana siku moja tuishi tena kama zamani, jambo ambalo kila mmoja angetamani lifikie.


Kama hakutakuwa na umakini halafu ikaonekana kuna madhara, maana yake hakutakuwa na nafasi ya kurejea kwa vitu vingine.


Hivyo, kuaminiana kwa mujibu wa utaalamu wa kila mtu, kuona usahihi na kufanya kwa kufuata weledi kuanzia kwa wachezaji, kwa maana ya kuwa wajikinge, wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya ni muhimu sana.


Mfano wachezaji watalazimika kufuata maelekezo ya wataalamu wengine tofauti. Zamani ilikuwa ni walimu pekee, lakini sasa ni wataalamu wa afya ambao wanakuwa sehemu ya maisha yao ya mchezo.



Tushirikiane pamoja ili tuweze kufanikisha nia njema ya Rais Magufuli, mwisho ikiwezekana kila kitu kirejee sahihi kabisa.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.