BEKI wa kulia wa Yanga, ambaye ni nahodha msaidizi, Juma Abdul, ameupongeza uongozi wa timu hiyo katika harakati zake za kutaka kuwasajili Relliants Lusajo ambaye ni mshambuliaji wa Namungo na beki wa kushoto wa Polisi Tanzania, Yassin Mohamed.
Imekuwa ikielezwa kuwa, Yanga inazifukuzia saini za nyota hao katika njia ya kukiboresha zaidi kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao.
Abdul amebainisha kuwa, mpaka sasa ana uhakika nyota hao watatua Yanga na kufanya nao kazi msimu ujao.Aliongeza kuwa, wachezaji hao wamekuwa na mwenendo mzuri kila kukicha, hivyo anaamini wataongeza nguvu kubwa kikosini hapo.
“Tangu nianze kusikia tetesi za uongozi kutaka kumsajili Lusajo na Yassin, nimekuwa nikiunga mkono kwa asilimia zote, kwani ni wachezaji wazuri, Lusajo tulishawahi kuwa naye Yanga, hivyo anaifahamu vizuri changamoto yake, ila hata hivyo utaona Yanga ilimuacha si kwa ubaya isipokuwa kocha wa kipindi hicho alikuwa na mastraika wengi.
“Yassin yeye nilianza kumkubali tangu alipokuwa Ndanda FC, hivyo naujua uwezo wake, labda tu itokee asajiliwe na ashindwe kuwa sehemu ya chaguo la kocha, ila kama kocha atampatia nafasi nina imani na uwezo wake,” alisema Abdul.
Chanzo: SpotiXtra
Post a Comment