Na Saleh Ally
WAKATI akisajiliwa Yanga, Kocha Mkuu wakati ule, Mwinyi Zahera alijigamba kuwa mshambulizi wake mpya, David Molinga atawaonyesha kazi.

 Baada ya muda, alimuweka kando na kuamua kumfanyisha mazoezi ya ziada akisema aliona alikuwa na uzito wa juu zaidi kuliko kiwango chake.

Molinga alirejea Yanga na kuanza kucheza wakati tayari ligi ikiwa imeanza na angalau alianza kuonyesha cheche zake taratibu akifunga mabao kadiri muda unavyosonga mbele.

Kwa sasa Molinga ni kati ya wachezaji wasiotakiwa Yanga na inaonekana hafai, wengi wakidai kwamba Yanga waliingizwa mkenge kumsajili.

Hili limechukuliwa na wanaoanzisha mambo na kuwapa pasi wanaoweza kuendeleza na sasa gumzo ni kwamba Molinga hafai. Lakini binafsi inanishangaza sana, si jambo la kawaida. Naona kama watu wamekuwa na haraka sana katika hili na wanapaswa kuliangalia upya.

Si sahihi kumhukumu Molinga kwa hisia na mawazo yetu binafsi badala yake tuangalie kazi yake ikoje. Kama unakumbuka uliwahi kuona video baadhi ya mashabiki wa Yanga wasiojitambua wakimzomea mchezaji huyo akiwa katika mavazi yake ya kawaida.


 Iliniumiza sana, nilishangazwa kuona mashabiki wa klabu fulani wanashindwa hata kuujua mchezo wanaofurahia ili mtu awe bora anahitaji jambo lipi! Vipi unamzomea askari wako katikati ya vita na kitu kibaya zaidi ndio ameanza kulitumikia jeshi lako.

Huu ni msimu wa kwanza, hadi sasa kama utafuata takwimu ni mchezaji wa kwanza kabisa anayepaswa kubaki Yanga kama kutakuwa na utaratibu wa kuangalia katika ushambulizi nani abaki nani aondoke.

Ana mabao nane, akiwa ndiye anaongoza kwa mabao ya kufunga licha ya kuchelewa kuanza kucheza na unaona takriban mechi sita hivi za mwishoni, amekuwa akiwekwa jukwaani.

Pamoja na hivyo, ndiye mfungaji bora zaidi katika kikosi cha Yanga katika Ligi Kuu Bara na katika ligi hiyo, anashika nafasi ya tano kwa maana ya idadi ya mabao. Maana anayeongoza Meddie Kagere ana mabao 19, wanaofuatia ni watatu wana mabao 11 kila mmoja, wa tatu ana mabao 10, wa nne ambaye ni Peter Mapunda wa Mbeya City ana tisa, anafuatia Molinga mwenye nane, sawa na Obrey Chirwa wa Azam FC na Daruwesh Saliboko wa Lipuli FC.

Si ajabu kwa sasa ukasikia watu wakimsifia Saliboko kwa kazi nzuri, bila ya kujali analingana mabao sawa na Molinga, tena Saliboko akiwa anacheza katika timu isiyokuwa na presha kama ilivyo kwa Yanga.

Pia si ajabu kuwasikia Yanga wakiwa na mpango wa kumrejesha Chirwa kutokana na kumuona mkali lakini amecheza mechi nyingi zaidi ya Molinga, leo wanalingana mabao ya kufunga. Na kikubwa zaidi, Chirwa leo ana misimu zaidi ya miwili katika Ligi Kuu Bara wakati Molinga hajamaliza hata msimu mmoja na anaonyesha kuwa na mwendelezo mzuri kabisa.

Wachezaji tunaowasifia na kuwaona wakali mfano Ayoub Lyanga wa Coastal Union ana mabao saba na amecheza mechi nyingi kama ilivyo kwa Kelvin Kongwe Sabato wa Kagera mwenye mabao sita. Simba wana John Bocco mwenye mabao manne, huenda sasa ana mechi sawa na Molinga au anamzidi lakini wanaendelea kumpa moyo na kujivunia wakiamini atafanya vizuri tu, vipi Yanga wanashindwa kwa Molinga!

Tabia ya namna hii ambayo iko njiani kumng’oa Molinga Yanga imekuwa ikizikosesha wachezaji sahihi klabu hizi kubwa hasa Yanga na Simba na wakati mwingine nimekuwa nikifikiria vibaya huenda kwamba kuna wale wanaofanya kwa maslahi yao.

Kwamba kuna mtu anataka mshambuliaji wake asajiliwe Yanga na anajua akisajiliwa ni maslahi kwake atapata fedha, anaanzisha kampeni za chinichini kuonyesha mshambuliaji fulani hafai, hivyo aondoke. Akifanikiwa anasajiliwa aliyemtaka yeye, inayoumia ni klabu.

Leo naendelea kushangazwa na Yanga kuona Yikpe Gnamien anapata namba ya kuanza huku Molinga akibaki benchi. Kwangu naona si sawa kwa kuwa kama Molinga angezidi kupata mechi za kucheza, angezidi kuwa bora zaidi kwa kuwa msimu huu ungekuwa bora kwake kuendelea kuzoea mazingira na kujiamini na ingewezekana kabisa akawa tishio kwa wengine msimu ujao.

Nawashauri mashabiki wa mpira, mchezo huu wa soka zaidi unapimwa na takwimu, msikubali kudanganywa kwa maslahi ya wengine, pimeni wenyewe kabla ya kuanza kuwashambulia watu wenu

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.