MABOSI wa Simba wameamua kumpa majukumu mazito kocha wao, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ya kuamua kumbakisha kiungo Msudan, Sharaff Shiboub ambaye mkataba wake unamalizika hivi karibuni.
Simba wamempa zigo hilo Sven la kutamka kuwa anamuhitaji kiungo huyo au kuachana naye kufuatia mchango ambao ameuonyesha hadi sasa ndani ya timu hiyo.
Shiboub alisaini mkataba wa mwaka mmoja wa kucheza Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan ambapo hadi sasa amehusika katika mabao nane akifunga mawili na kutoa pasi sita za mabao.
Habari zinaeleza kuwa, Sven ndiye ameachiwa suala hilo ambapo kauli yake ndiyo ambayo itaamua kiungo huyo Msudan aendelee kubaki klabuni hapo au la.
“Kila kitu kwa sasa kuhusu timu kiko mikononi mwa kocha Sven, yeye ndiye ambaye ataamua nani na nani waondoke na wachezaji gani pia wabaki kwa ajili ya msimu ujao.
“Hata hilo kuhusiana na kusaini mkataba mpya limeachwa mikononi mwa Sven, hata wachezaji wengine pia juu ya mustakabali wao utabaki kwa kocha na kwa kuzingatia takwimu za kila mchezaji alichokifanya,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema: “Kuhusiana na wachezaji wote juu ya mikataba yao na nani ataondolewa suala hilo lipo mikononi mwa kocha wetu mkuu,".
Post a Comment