Na Saleh Ally
UPANDE wa mashabiki wa soka hasa wa hapa nyumbani Tanzania, moja ya vipindi ambavyo huvifurahia ni vile vya usajili wa wachezaji wapya.

Vinakuwa viwili, mwishoni mwa msimu wakati maandalizi ya msimu mpya yakianza. Baada ya hapo, ni kile kipindi cha dirisha dogo la usajili.

Mara nyingi kipindi hiki cha usajili wakati msimu umeisha, kinakuwa kitamu sana kwa mashabiki wa soka kwa kuwa timu hufanya usajili mkubwa tofauti na dirisha dogo ambapo huwa kwa ajili ya marekebisho.

Mashabiki wao wanachotaka ni burudani, kuona mtu mpya akisajiliwa, hasa akiwa na umbo kubwa, umbo la kipande cha baba na kadhalika, atakuwa gumzo hata kabla ya kuujua utendaji wake. Bado watafurahia tu.

Kwa upande wa klabu, kama weledi utakuwa unafuatwa, kuna mengi ya kuangalia wakati mchezaji mpya anakuwa anasajiliwa.

Kwanza kabisa awe msaada katika kikosi, hili ndilo lengo kwa kuwa inakuwa ni kujenga kwa matofali bora nyumba iwe imara. Timu inatakiwa kuwa imara ili ifanye vizuri.

Pili ni kuangalia thamani ya kile klabu inachokipata kwa ajili ya timu yake kwa kuwa kuna gharama. Hili ni jambo muhimu unapoangalia matumizi na mapato na mara nyingi, matumizi lazima yawe na faida lakini matumizi lazima yafanywe kwa umakini mkubwa. 

Hakuna sababu ya kusajili mchezaji kwa fedha nyingi halafu baada ya nusu msimu anaonekana hana faida yoyote kwa timu, yanaanza yale mambo ya afadhali angekuwa fulani au uongozi ulikurupuka.

Wanaohusika na usajili lazima wafuate weledi, lazima waijue kazi yao na katika usajili hakupaswi kuingia siasa ya watu kutaka kufanya kwa ajili ya furaha au matumbo yao.

Hapa pia nataka kuilenga Yanga, ukiangalia kwa wachezaji hasa wa nje, Yanga imesajili wachezaji zaidi ya 14 ndani ya msimu mmoja na unaona kati ya hao nusu yake imewaacha hata kabla ya kukamilisha msimu.

Uliona usajili ule wa akina Issa Bigirimana, Sadney Urikhob, Juma Balinya na wengine. Baada ya hapo kukawa na marekebisho makubwa ya kupata wachezaji wapya. Lakini unaona karibu wote walioongezwa kwa mtazamo tu unaona wamesogea katika mlango wa kutokea.


Maana yake kuna uwezekano tena wale waliosajiliwa katika dirisha dogo, zaidi ya 60% nao wakaondoka pia na mpango ukawa ni kusajiliwa wachezaji wapya. Hii haitakuwa sahihi kwa afya ya kikosi ambacho kinahitaji mambo mengi sana unapozungumzia suala la usajili na wachezaji wapya baada ya usajili kukamilika.

Wachezaji wana aina tofauti, wapo ambao wana uwezo mkubwa sana wa kuzoea mazingira haraka na kuanza kutoa matunda yao lakini wapo ambao huhitaji muda kwanza ili waweze kufanya vizuri na bado wakawa bora zaidi hasa kama watapata huo muda.

Haya yote yanaweza kufanikiwa, kama kutakuwa na wataalamu ambao wanapewa nafasi ya kuyachakata mambo kitaalamu kulingana na hali halisi. Hawa watakuwa wang’amuzi, watakuwa wanatambua ubora wa mchezaji hata kama haujaanza kuchipukia na wakaaminika.

Kama itakuwa mchezaji akishindwa kutamba katika mechi mbili au tatu halafu ikaonekana ni dhambi kubwa na viongozi ndio wakawa wa kwanza kupitisha majungu chinichini, hii si sawa, katika hali ya kawaida inamfanya mchezaji kuzidi kuchanganyikiwa zaidi na huenda akaharibikiwa kabisa.

Hivyo hapa kuwe na mfumo unaotegemeana lakini imara kabisa. Wakati wa kutafuta wachezaji, kuangalia mahitaji ya kikosi lakini baada ya wachezaji kusajiliwa nini cha kuwasaidia ili wawe bora na kuweza kutoa matunda kwa faida ya klabu ambayo inakuwa imegharamika kumnunua au kumsajili.

Ndio maana nasema, kwa afya ya kikosi chao, huenda Yanga wanapaswa kuwa zaidi ya makini katika usajili huu kwa kuwa tayari inaonyesha wachezaji wengi kutoka katika nchi za Rwanda, DR Congo, Burundi, Kenya na kwingineko wangependa kucheza Yanga.

Kwa hapa nyumbani, ni kawaida pia bila ya ubishi, wachezaji wengi wanapenda kuitumikia Yanga kutokana na ukubwa wake.

Hivyo, kwa kuwa Yanga imekosea sana, hasa msimu huu, basi kwa kuwa unakwenda kwisha, lazima ionyeshe ilijifunza kupitia makosa ya msimu uliopita na sasa iko makini na kila usajili utakuwa na faida na msaada kwa klabu ili kuepusha hasara za kutoa fedha kwa wasio sahihi na kulazimika kumwaga tena fedha kwa wengine ili kurekebisha makosa.

 Bila shaka Yanga wanaweza kurekebisha hayo makosa kwa kuwa tumeona kupitia walichokifanya kwa Bernard Morrison, basi waendelee.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.