NA SALEH ALLY
SIKU moja nilikuwa nazungumza na kiungo mkongwe ambaye alipata nafasi ya kucheza na Hassan Dilunga wakati wakiwa Yanga, akaniambia yule ni mtu hatari sana! 


Kiungo huyo alikuwa akinielezea namna Dilunga alivyo na uwezo mkubwa tofauti na ambavyo tumekuwa tukimuona.


Moja ya swali nililomuuliza, “vipi awe bora halafu alichonacho kionekane mazoezini, kisionekane katika mechi sehemu ambayo anasubiriwa kuonyesha hicho alichonacho?”


Jibu lake lilikuwa hivi: “Dilunga bado hajajitambua, ninaamini kucheza Yanga au Simba kwake ni jambo la kujivunia na anaamini amefikia mwisho, jambo ambalo ni kosa.”


Juzi nimeona mahojiano ya Dilunga na gazeti namba moja la michezo la Championi, akisema anaona ni wakati wa kuondoka nchini na kwenda kucheza nje.


Katika mahojiano hayo, Dilunga alisisitiza kwamba angependa kwenda nje baada ya kuwa amekamilisha ndoto yake ya kuzichezea timu kubwa za Yanga na Simba.


Ameeleza kuwa ana taarifa za kuwa anatakiwa Yanga lakini angependa kucheza nje ya nchi. Hapa ninaweza kuwa nina maswali lakini vizuri kuendelea na kile alichokisema.


Kama ni swali ningeanza na kuhoji kama kweli Dilunga ana nia thabiti ya kwenda kucheza nje, au anafanya hivyo kwa ajili ya kutikisa kiberiti kwa kuwa angependa Simba kama wanamuongezea mkataba basi waweke donge nono zaidi?


Mara nyingi kwa wachezaji wa Tanzania wamekuwa wana mtindo huu, kwamba mkataba ukikaribia kwisha anaanzisha mazungumzo kuwa angependa kujiunga na timu fulani, tuliona hata alichokifanya Papy Tshishimbi kwa Yanga na wengine wengi.


Hii inakuwa tofauti na kwingine ambako mpira umeendelea ambako suala la mchezaji apate timu gani linaanzia na kampuni inayomsimamia na yeye anaongeza chachu kwa kucheza soka uwanjani, basi.


Kama Dilunga kweli ameamua kwenda kusaka maisha nje ya Tanzania, naweza kusema amebadilika au kupevuka zaidi na nimeyaamini maneno ya yule kiungo niliyezungumza naye kuwa Dilunga aliamini sana Yanga na Simba ndiyo mwisho wa safari yake.


Maana yake Dilunga ameamka, kile alichokisema yule kiungo ingawa hakumsikia wakati akiniambia, naye ameking’amua na sasa anataka kupiga hatua zaidi.

Kwa maana ya uwezo na kipaji, sote tunajua kwa Dilunga wala si suala la kuuliza. Anaujua na tumeona namna ambavyo hata akikaa benchi anavyoingia anachokifanya.

Pia unaona, makocha wa aina tofauti, kila kocha aliyepita Simba alimuamini kuanza au kuingia. Hakuwa akimuweka jukwaani.


Kitendo cha kucheza licha ya ushindani mkubwa wa namba Simba, inathibitisha kuwa ana uwezo wa juu na anachotakiwa ni kujisimamia katika juhudi na nidhamu.


Kumbuka, Dilunga alikwenda Mtibwa Sugar ambako aliiwezesha kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho na yeye akaibuka kuwa mchezaji bora wa msimu wa kikosi hicho.


Kuwa mchezaji bora pamoja na kuonyesha uwezo uwanjani kwa maana ya kuwa tegemeo au faida kwa kikosi, lazima utakuwa na nidhamu.


Nakumbuka yule kiungo niliyezungumza naye, pamoja na hivyo aligusia kitu kimoja, kwamba ana tatizo la uvivu wa mazoezi. Inawezekana ni wakati ule lakini kama hajabadilika basi ni lazima afanye hivyo.


Bila shaka kama atafanikiwa kupata timu nje ya Tanzania, basi lazima ajue suala la nidhamu lina tofauti kubwa na hapa nyumbani na linapewa kipaumbele sana.



Mchezaji hata awe na kiwango kinachomkaribia Lionel Messi au Cristiano Ronaldo, nidhamu ni namba moja. Kwa hata hao vinara wawili nao wana nidhamu ya juu wanapokuwa kazini. Hiki ndiyo Dilunga anapaswa kukisimamia.


Binafsi namuwekea msimamo, kwamba ninaamini ana uwezo wa kucheza kwa maana ya uwezo au kipaji alichonacho na anaweza kung’ara nje na thamani yake ikawa juu sana kama atasimamia juhudi, maarifa na kutanguliza nidhamu.


Kama aliweza Mtibwa Sugar hadi kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu, maana yake mambo haya si mapya tena kwake na yanawezekana.


Tanzania inahitaji vijana wanaocheza nje, watakaojifunza mambo mapya na kubadilika kimawazo ili waongeze nguvu kwenye timu ya taifa lakini katika soka la Tanzania pindi wakaporejea nyumbani kumalizia soka lao kama wachezaji au wakiamua kuwa makocha. Go, tembea uende Dilunga

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.