UONGOZI wa Arusha FC,(AFC) inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF) kuwakumbuka katika wakati huu wa janga la Corona kwa kuzipa sapoti timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Ligi Kuu Tanzania Bara ilisimamishwa na Serikali ili kuchukua tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona Machi 17 ila kuna matumaini ya kuweza kurejea mwezi Juni jambo ambalo linawapa wasiwasi viongozi wa AFC namna watakavyomaliza ligi.
Akizungumza na Saleh Jembe, Ofisa Habari wa AFC, Bahati Msilu alisema kuwa janga la Corona limetibua mipango ya fedha kutokana na wao kutegemea watalii ambao hawakuwepo kwa muda mrefu.
“Ujue shughuli nyingi zilisimama na AFC hatukuwa na hesabu nyingine za kukusanya fedha hasa ukizingatia tulikuwa tunategemea masuala ya utalii, pia tulikuwa na matatizo ya kuwarudisha wachezaji wetu makwao baada ya kambi kuvunjwa hapo tumeyeyusha fedha nyingi.
“Bajeti yetu kwa sasa hata sielewi ipoje maana tayari ilishayeyuka wakati wa janga la Corona, ombi langu kwa TFF wasitusahau pale ligi itakaporejeshwa hali huku ni tete kwa timu nyingi za madaraja ya chini ukizingatia hakuna wadhamini,” amesema Msilu.
AFC ipo nafasi ya sita ikiwa na pointi 25 kibindoni baada ya kucheza mechi 18 ndani ya kundi B ambalo kinara wake ni Gwambina mwenye pointi 40
Post a Comment