KWANZA kabisa napenda kuipongeza Serikali yetu iliyo chini ya Rais Dk John Magufuli kwa hatua mbalimbali za awali za kujihadhari na maambukizi ya Ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona, ambavyo tangu kulipuka kwake vimekuwa janga ambalo limebadilisha mustakabali mzima wa maisha ya binadamu duniani kwa sasa.
Hatua ya kuamua kusitisha kwa muda wa siku 30 mikusanyiko yote hasa ile isiyokuwa na ulazima iliyotangazwa na Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni ya kupongezwa kwani kama ambavyo tumesikia moja kati ya njia ambazo ugonjwa huu husambaa ni kupitia hewa.
Pili napenda kuipongeza TFF na Bodi ya Ligi kwa utekelezaji wa maazimio hayo ya Serikali kwa kuamua kusitisha michezo ya ligi zote ambazo ziko chini ya TFF na bodi hiyo kwa siku 30 hii ni hatua nzuri katika mapambano haya dhidi ya Corona na inastahili pongezi.
Baada ya maamuzi haya ya TFF na Bodi ya Ligi tumesikia kuwa klabu nyingi zimelazimika kuvunja kambi zake na kuruhusu wachezaji wao ‘wakajikarantini’ majumbani mwao huku wakisubiri taarifa mpya kutoka TFF hasa baada ya hizi siku 30 kuisha.
Swali kwa klabu zetu ni kuwa baada ya kuvunja kambi je, wamewaruhusu wachezaji hao kutoka nje ya mipaka ya Tanzania? Na kama wamewaruhusu je, huko waendako ni sehemu salama? Na je, ni tahadhari gani ambazo wanazichukua wakiwa huko?
Ni muhimu kuuliza maswali haya kwani tumesikia baadhi ya wachezaji wa kigeni tayari wameondoka na wako nje ya nchi kwa maana wamerudi nchi zao za asili.
Wachezaji kama Meddie Kagere wa Simba inaelezwa yuko kwao Rwanda na David Molinga, straika wa Yanga inaeelezwa kuwa yupo Ufaransa.
Kumekuwa na hofu juu ya majaliwa ya wachezaji hawa na hata baadhi ya makocha katika suala la wao kurudi nchini hasa baada ya TFF kupitia kwa Rais wake, Wallace Karia kutoa tamko kuwa nyota hawa hawataruhusiwa kurudi nchini, hapa ipo haja ya hekima kutumika katika suala hili.
Tunatambua kweli lilitolewa zuio la wachezaji kutotoka nje ya nchi lakini hao tayari wamekwenda kwao, kwa hiyo kama itatokea wakirudi basi hekima itumike kwa kuwapima na kuwaweka karantini kwa ajili ya kuzuia maambukizi kwa wenzao.
Mwisho kabisa napenda kuwakumbusha wachezaji wanaokipiga katika klabu mbalimbali nchini kukumbuka kuwa wapo vitani hivyo likizo hii ya ghafla isiwafanye wakajisahau na kwenda kuponda raha bila kufanya mazoezi ili kuendelea kujiweka fiti.
Kwani kama wataangukia katika mtego huo wa kula bata bila matizi ni dhahiri kuwa watakuja kuzigharimu klabu zao pindi Ligi itakaporejea.
Lakini kwa nafasi ya pekee sana tuendelee kuwakumbusha wachezaji wetu ambao walikuwa katika kambi ya Taifa Stars kuwa bado nchi inaendelea kuwategemea.
Hivyo likizo hii iwe sehemu ya kuongeza utimamu wao wa mwili kama ambavyo kocha Ettiene Ndayiragije amewaagiza na atakayekiuka ni dhahiri kuwa atapoteza nafasi yake.
Post a Comment