Kitu gani kinawatesa Singida United? Hilo ni swali gumu au kitendawili kigumu kukitegua kwa watu.
Kinaweza kikawa kitendawili kigumu kukitegua kwa sababu moja tu sisi Watanzania hatuupendi ukweli ndio maana wengi wanaamua kujikalia kimya tu.
Ndio hatupendi ukweli, ni watu tunaondekeza uongo kwa minajili ya kujipendekeza, hilo ndilo tatizo letu na nimewahi kusema hapa kwa mtindo huo soka letu litadidimia.
Wengi wanajua kinachowatesa Singida United na kuna timu zipo za namna hiyo na zinatesa hivi sasa ingawa hatujui mwisho wake kama unaweza ukawa kama huu wa Singida United.
Siku zote ninasema tatizo la soka letu ni mifumo ambayo siyo rasmi ndiyo inalitesa soka la Bongo na wengi tunaiacha tu iendelee kunawiri.
Wenyewe hatuna habari, tunaachwa tu ilimradi siku zinasonga, hii ni hatari sana kwenye nchi kama hii inayopigania kulipandisha soka lake kwenda mbali zaidi.
Singida United inaburuza mkia, yaani ni ya leo kesho kama vile mgonjwa aliye mahututi pale kwenye Hospitali ya Muhimbili.
Kutoka kwenye timu pendwa hadi kuwa timu ya kubangaiza hili linauma sana, siyo kwa Singida United yenyewe tu bali kwa soka letu lote.
Hili tusiliache hivihivi likapita, lazima tukae chini tulijadili kwa kina ili kulipatia ufumbuzi, yaani kama nilivyosema huko juu kuna timu zinakuja au zipo kama Singida United.
Tukiliachilia hivihivi likapita, miaka michache ijayo tutakuwa na kilio kingine kama hiki cha sasa hivi cha Singida United.
Kwani wewe unadhani Singida United ni timu mbaya? Si kweli, bali ni timu nzuri yenye kocha mzuri wa kiwango cha juu, lakini kuna mambo yanawatatiza na ndiyo yanawafanya wawe hapo walipo.

Singida United iliyokuwa na wadhamini lukuki, leo inahangaika haijui pakushikia, inasikitisha sana, tena sana.
Hapa kuna cha kujifunza na kulichukulia hatua ili tutengeneze mfumo sahihi wenye maslahi kwa soka letu na lazima tuwe wa kweli katika hili.
Tuache kuingiza siasa kwenye soka, hilo nalo lazima tuliseme maana kuna wanasiasa wanalichukulia soka kama mtaji wao wa kisiasa ili kujitengenezea njia ya mafanikio.
Kama hilo hatuwezi kulikemea tena kwa muda huu ninawahakikishia hatuwezi kufika popote, tutazungukazunguka tu basi hakuna lolote la maana.
Tukifanikiwa katika kuitenga siasa na soka, tutafika mbali sana kwani vitu hivi viwili haviwezi kwenda sambamba na kuibuka na mafanikio.
Hivi hawa wanasiasa wanatuchukuliaje sisi wanamichezo? Mbona wanapokuwa na shida ya jambo lao ndiyo wanajisogeza zaidi kwetu, wakishalipata wanakimbia.
Tunatakiwa kubadilika ili kuliokoa soka letu, nasema hivyo kwa sababu leo hii Singida United, kesho itakuwa kwa timu nyingine, timu hizo zitakuwa zikiliwa na wanasiasa, mwisho wa siku tutakosa timu imara ya kuiwakilisha nchi kimataifa.
Kwa muda mrefu timu zetu za klabu zimekuwa zikihangaika katika kusaka matokeo mazuri zinaposhiriki michuano ya kimataifa.
Itazame KMC ambayo msimu uliopita ilifanya vizuri ilipopanda daraja, siasa ilipokolea, nayo ikapotea, leo hii nayo ipo hatarini kushuka daraja

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.