KAMA inavyojulikana, mashindano yote ya kimichezo, ikiwemo Ligi Kuu Bara, yamesimamishwa kwa muda kupisha janga la Virusi vya Corona, linaloendelea kuitesa dunia kwa kasi kubwa.
Tumeshuhudia baadhi ya watu maarufu wa Tanzania wakibainika kuwa na Virusi vya Corona, akiwemo msanii wa Bongo Fleva, Mwana FA na Meneja wa Diamond Platnumz, Sallam SK.
Kipindi hiki ambacho ligi imesimama, kama wachezaji wasipokuwa makini, wanaweza kurejea uwanjani wakiwa na viwango duni.
Hiki siyo kipindi cha wachezaji kujisahau. Na kama wakithubutu kufanya hivyo, basi kutakuwa na anguko kubwa sana katika viwango vya soka mara ligi itakaporejea.
Wakati ligi zikiwa mapumzikoni na timu nyingi zikiwa zimevunja kambi, kwa wachezaji wanaojielewa, huu ni muda wa kufanya mazoezi ya binafsi kila siku ili kutunza kiwango chao.
Huku wakiwa wamejitenga kutokana na mlipuko wa virusi vya Corona na wakiepuka mikusanyiko, huu ni wakati wa wachezaji kuendelea kujenga stamina zao na kuboresha zaidi viwango vyao kwa mazoezi makini.
Shida ya baadhi ya wachezaji wa Kibongo, hii kwao ndiyo fursa ya kujirusha na kusahau kabisa mambo ya kimichezo, kama kuna mchezaji atafanya hivyo ajue kabisa anajimaliza mwenyewe.
Mchezaji makini hawezi kusahau mazoezi katika kipindi hiki.
Atahakikisha anafanya mazoezi kwa nguvu zaidi kwa kuwa hakuna mechi ya kimashindano ya kucheza, na tunajua kwamba kama hakuna mechi, maana yake inatakiwa zifanyike juhudi za ziada kulinda kiwango.
Mchezaji anapocheza ndiyo hulinda kiwango, lakini asipocheza, maana yake anatakiwa afanye mazoezi ya ziada ya kulinda kiwango.
Mpira siyo kama baiskeli kwamba ukishaelewa kuendesha, hata usipoendesha miaka 20, siku ukiendesha hautaanguka.
Mpira ni sayansi, ili uwe bora, unatakiwa kufanya mazoezi sana.
Hivyo ndivyo, tumekuwa tukishuhudia kila siku kwa akina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, Mbwana Samatta na wengine, wanapokuwa katika mapumziko, hawasahau mazoezi, licha ya kuwa wana vipaji vikubwa.
Utaona mfano kwa sasa Ronaldo amejitenga kwao Ureno akiwa na familia yake, lakini kila siku amekuwa akijifua zaidi na zaidi.
Mchezaji hauwezi kuwa bora kama hautafanya mazoezi, hata kama una kipaji cha namna gani. Mazoezi ni lazima.
Wachezaji wasipofanya mazoezi kipindi hiki, wakaishia kufanya anasa tu, ligi itakaporejea, tutashuhudia wengi wao wakiwa chini ya viwango, maana yake tutakosa soka la kuvutia katika ligi yetu.
Hatutaki hilo litokee, tunataka kuona soka likichezwa kwa kiwango cha juu. Siri ni kutokulala wakati huu wa mapumziko, ukilala ujue kuwa na soka lako litalala.
Corona isiwe sababu ya kuua kipaji chako, kuna namna ya kufanya ili kukilinda kipaji ulichonacho, ili kuendelea kuwa hazina kubwa kwa taifa.
Post a Comment