MAMBO ni moto! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa vinara wawili wa Bongo Fleva ambapo Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amejikuta kwenye wakati mgumu, kisa wimbo wa zamani wa mwanamuziki mwenzake, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’.
Ilikuwa hivi; wikiendi iliyopita, Diamond au Mondi alitupia kipande cha video kwenye ukurasa wake wa Instagram kupitia Insta Story akiuimba wimbo huo wa Kiba uitwao Hadithi na kuusifia kwamba ni mzuri.
WIMBO WAMPONZA
Kutokana na kusema anaupenda wimbo huo, mashabiki ambao ni Team Kiba walikerwa na kitendo hicho na kudai kuwa alikuwa anamchora ‘Mfalme’ wao hivyo walimshambulia Mondi vilivyo huku wengine wakimuuliza anamtafuta nini Kiba kwa sababu amekuwa akimfuatafuata mara kwa mara.
“Hivi wewe…(linatajwa jina baya la kumdhalilisha Mondi juu ya maumbile yake) hukomi mpaka uje kupigwa na Kiba ndiyo utamkoma, mtu amekuambia hataki shobo zako muache,” aliandika mmoja wa wafuasi kwenye mtandao huo wa Instagram.
NI MAPENZI TU
Licha ya wengi kumshambulia Mondi kwa matusi yasiyoandikika gazetini kutokana na hilo, wapo waliompongeza wakisema kuwa anafanya hivyo kwa kuwa ana roho safi, yaani hana chuki na msanii mwenzake King Kiba ndiyo maana kila wakati amekuwa akimsapoti kwenye kazi zake.
“Diamond anaonekana hana kinyongo na King Kiba ndiyo maana amekuwa akijishusha na kufanya yote hayo, yaani ni mapenzi tu hakuna kingine,” aliandika shabiki mwingine anayeitwa Nancy.
TUJIKUMBUSHE
Mondi mara nyingi amekuwa akisapoti au akimzungumzia sana Kiba hasa kwenye kazi zake kimuziki kwani amekuwa akipiga nyimbo zake kwenye runinga na redio yake ya Wasafi huku akimualika kwenye tamasha lake la Wasafi.
Kama hiyo haitoshi, pia wanapokutana, Mondi hujishusha na kumsalimia Kiba, lakini Kiba hukataa salamu yake kama ilivyokuwa kwenye msiba wa aliyekuwa video queen maarufu Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ pale Leaders Club, Kinondoni jijini Dar.
Post a Comment