HARUNA Niyonzima, kiungo wa Yanga amesema endapo Ligi Kuu Bara itarejea timu yake ina uhakika mkubwa wa kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika au Ligi ya Mabingwa Afrika.
Niyozima ameweka wazi hayo ikiwa ni siku chache baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt Hassani Abassi, kusema kuwa tayari Serikali imeshakutana na Baraza la Michezo na kupokea mapendekezo yote ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), huku akiwahakikishia wadau kuwa ligi itarejea siku si nyingi.
Niyonzima amesema kama Yanga itacheza michezo yote iliyosalia bila kusimama, basi watakuwa na uhakika wa kutwaa Kombe la Shirikisho (FA) na hata kupata nafasi ya pili kwenye ligi ambayo pia inaweza kuwapa nafasi ya kucheza michuano hiyo.
“Kusimama kwa ligi kumetoa nafasi kubwa kwa klabu zote kupumzika hivyo, ligi ikianza hakutakuwa na klabu ambayo imecheza michezo mingi zaidi ya nyingine, hivyo viwango pekee vya wachezaji binafsi ndivyo vitaamua nafasi ya kumaliza ligi.
“Sisi tunajivunia zaidi mifumo mizuri ya kocha wetu na kwamba amekuwa akituhimiza mara kadhaa namna ya kujiweka sawa kabla ya ligi kurejea, hivyo kila mchezaji ana hamu ya kurejea uwanjani na kusawazisha mapungufu yote yaliyojitokeza kabla ya kusimama kwa ligi, naamini tutarejea na nguvu na kuchukua Kombe la Shirikisho au kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi,” amesema Niyonzima
Post a Comment