KOCHA mkuu wa Yanga, Mbelgiji, Luc Eymael amesikia ishu ya Simba kumfukuzuia mshambuliaji wa Rayon Sports, Mghana Michael Sarpong.
Kumekuwa na tetesi za Simba kuingia kwenye vita za kuwania saini ya nyota huyo ikiwa ni siku chache kupita tangu mshambuliaji huyo kukiri kufanya mazungumzo na Yanga kupitia wakala wake Alex Kamanzi, ambaye aliwaambia Yanga watoe kiasi cha dola 100,000 ( sh milioni 230 za Kibongo) ili waweze kupata saini yake.
Yanga imekuwa ikipambana kutaka kuwania saini ya mshambuliaji huyo mwenye uwezo wa kucheza nafasi za winga zote kupitia kwa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said, ambao ni wadhamini wa Yanga.
Eymael amesema kuwa kwa upande wake anaamini uongozi wa timu hiyo utahakikisha mshambuliaji huyo anatua ndani ya kikosi chake kwa kuwa amekuwa kwenye mipango yake.
“Suala la kumtaka na wao Sarpong haliwezi kunishangaza lakini naamini viongozi wangu ambao wamekuwa wakishughulikia mambo ya usajili watamaliza hilo kwa sababu huyo mchezaji yupo kwenye mipango yangu sasa haitokuwa rahisi kukubali tumuache kwenda Simba.
“Binafsi sikupata mshtuko kusikia Simba wakimtaka lakini haitokuwa rahisi kuweza kumchukua na ukiangalia sioni shida ya washambuliaji kwao maana wana Meddie Kagere halafu wana John Bocco, nadhani wanataka kuvuruga mipango yetu ila naamini Sarpong hawezi kwenda kwao na wanatakiwa washughulikie matatizo yao na siyo ya timu yangu,” amesema Eyamel
Post a Comment