NA SALEH ALLY
NIMESHANGAZWA sana kuhusiana na wadau wengi wa mchezo wa soka kuonekana kufurahia baada kuwepo kwa taarifa ya ufujaji wa fedha na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutajwa.
Furaha hiyo naiona katika makundi mengi ambayo kuna wadau wa soka ambako mijadala inaendelea lakini waziwazi inaonyesha haina mizizi ya kutosha kuanza kukua.
Hii ni baada ya Brigedia Jenerali, John Mbungo ambaye ni Mkurugenzi wa Takukuru kusema anajua kuwa fedha Sh bilioni moja wakati wa michuano ya Afcon ya vijana nchini zilitumika vibaya na uchunguzi unaendelea vizuri.
Brigedia Mbungo alisema wahusika wanaitwa, wanahojiwa na wamekuwa wakiitwa kwenda Takukuru kufanya hivyo. Pia alielezea kuwa wahusika wanapewa nafasi ya kurudisha fedha hizo kwanza.
Wakati mkuu huyo wa Takukuru akijibu swali hilo kama utakuwa makini utagundua hakuna sehemu aliitaja taasisi au mtu. Hakusema TFF, ofisa wake au shirika fulani linahusika badala yake alitumia neno “wahusika”.
Baada ya hapo, ikaibuka hiyo furaha ya watu wengi wakisema wametajwa, jambo ambalo ukitilia, muuliza swali aliwataja TFF wakati akiuliza swali.
Wakati katika makundi ya WhatsApp na mitandao ya kijamii watu wakiendelea kuwataja TFF, wao wakaamua kutoa taarifa wa vyombo vya habari na mwisho wakasema kwamba fedha Sh bilioni moja zilizotolewa hazikuingia katika akaunti ya TFF, hivyo wapo ambao ni sahihi wanapaswa kuzijibia.
Nilimsikia Rais wa TFF, Wallace Karia akihojiwa na TBC, yeye akasema kwa mara nyingine fedha hizo hazikuingia katika akaunti ya TFF huku akionekana kuwapongeza Takukuru kwamba wafanye kazi yao na yeye yuko tayari kutoa ushirikiano kama atatakiwa.
Karia amesema amekuwa akikerwa na tuhuma hizo kiasi cha kufikia kutukanwa na baadhi ya wadau, hivyo ni wakati mzuri wa kupata uhakika kwa kuwa yeye anajiamini lakini ikibainika kuna tatizo, iwe kwake au ofisa mwingine wa TFF, basi achukuliwe hatua.
Umakini unahitajika sana katika hili, la sivyo tunaweza kutengeneza ambayo hayahusiki, tunaweza kuanzisha ambayo si sahihi kutokana na mihemko ambayo imeanza kuonekana mapema kama vile watu wanafurahia TFF nayo kuonekana imekosea.
Tangu TFF wameingia madarakani, suala la udhibiti wa masuala ya fedha limekuwa kubwa. Wamekata mirija mingi ya wale ambao walikuwa wakifaidika sana na shirikisho hilo na wamejiwekea uongozi wenye misingi au ugumu.
Huenda kama unafanya vizuri kwa muda mwingi na ilizoeleka sehemu uliyopo huwa inaharibu sana, huenda watu huwa wanatamani kukuona unaharibu, hili ndilo linaonekana kujitokeza katika kipindi hiki.
Kama mtu anafanya vizuri na mambo yanaonekana, ni vizuri kumpongeza na kama ameharibu na una nafasi ya kusema kwa nia ya kujenga ni vizuri lakini katika tuhuma ni vizuri kuwa makini.
Wakati wa kuzungumza tuhuma lazima kueleza mambo kadhaa kama anatuhumiwa, imeelezwa na kadhalika badala ya kusema kwa kulazimisha ukisema “ameiba”, “mwizi” na kadhalika kwa mwisho wa uchunguzi, kunaweza kukuletea shida.
Kama ambavyo nimesema Brigedia Mbungo hakusema TFF sehemu yoyote zaidi ya kuelezea uchunguzi unaendelea na upo pazuri na wahusika wameanza kuhojiwa.
Vizuri kuwapa nafasi Takukuru waifanye kazi yao kwa weledi na baada ya hapo, watakuja kutueleza kilichopo kwa kuwa wanaijua kazi yao vizuri.
Kuanza kuwashambulia TFF kishabiki kwa sasa ni kuonyesha chuki binafsi. Kuonyesha furaha baada ya kusikia wamekosea ni kuonyesha pia huenda kuna ubora wa jambo wanalifanya, linawakera wengi ambao hawafaidiki tena au mirija imezibwa.
Tuwaachie Takukuru, wakimaliza hapo tutakuwa na nafasi ya kuwajua waliofanya ubadhilifu huo na wakati sheria ikichukua mkondo wake, kutakuwa na nafasi ya kujadili.
Na kama hukumu ikipita, itakuwa nafasi nyingine ya onyo kwa wanaotumia hovyo fedha za maendeleo ya soka na kuliacha limechakaa. Hapa tutasema tutakavyo kwa aina tunayotaka sasa
Post a Comment