KIUNGO mshambuliaji wa kikosi cha Simba, Miraji Athumani ‘Sheva’, ameonekana kuanza kurejea kwenye ubora wake akitokea kwenye maumivu ya misuli.
Sheva yupo nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi miwili akiuguza maumivu hayo aliyoyapata akiwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichokuwa kinashiriki Cecafa nchini Uganda.
Kiungo huyo ni kati ya wachezaji waliojiunga na Simba kwenye msimu huu akitokea Lipuli FC ya mkoani Iringa ambaye alianza na kasi kubwa ya kufunga mabao sita kabla ya kuumia.
Staa huyo alionekana katika mazoezi ya pamoja na nyota wakubwa wanaocheza Ligi Kuu Bara kwenye Ufukwe wa Sea Scape uliopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Kiungo huyo alionekana akifanya program zote za mazoezi ya viungo huku akikimbia mbio fupi na ndefu akiwa na baadhi ya wachezaji wenzake wakubwa Haruna Niyonzima, Juma Kaseja, Said Ndemla, Hassani Isihaka, Shaaban Kado na wachezaji wengine wanaochipukia.
Mara baada ya kumaliza programu hizo, vikapangwa vikosi viwili na kucheza mechi, wakati mazoezi yakiendelea Sheva alionekana kupiga mashuti ya mbali huku akikokota mpira kwa kutumia miguu yote miwili.Mechi hiyo ikiendelea, Sheva alifunga bao kwa shuti la umbali wa mita 18 ambalo halikudumu baada ya Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kusawazisha kwa kumchambua Kado ndani ya sita
Post a Comment