MIRAJ Athuman,’ Sheva’ ni mzawa anayekipiga ndani ya Simba ambaye ni ingizo jipya kwa msimu wa 2019/20 akitokea ndani ya Lipuli.
Sheva hakuwa na mbwebewe sana wakati wa usajili wake wakati mastaa ikiwa ni pamoja na Ibrahim Ajibu, Deo Kanda , Wilker da Silver, Tairon Santos , Gerson Fraga na mastaa wengine walitambulishwa saa saba ila yeye akaona isiwe tabu akapiga picha nyuma ya bango na kuiachia kwenye mitandao ya kijamii.
Hakutambulishwa kama mastaa wengine ila muda aliotumia uwanjani na mambo aliyoyafanya ni maajabu makubwa kwani anaonyesha ana kile kipaji kutoka moyoni.
Simba ikiwa imefunga mabao 63 kwenye Ligi Kuu Bara amehusika moja kwa moja kwenye mabao tisa ambapo amefunga mabao sita, pasi moja ya bao na amesababisha penalti mbili.
Hatua kwa hatua SpotiXtra inakuletea maajabu ya Sheva ndani ya uwanja kitaifa na kimataifa twende sawa.
Mabao yake haya hapa
Bao lake la kwanza aliwatungua JKT Tanzania, Agosti 28 Uwanja wa Uhuru kwa kichwa dakika ya 73 akimalizia pasi ya Meddie Kagere.
Bao la pili aliwatungua Mtibwa Sugar ilikuwa Septemba 19, Uwanja wa Uhuru kwa guu la kushoto dakika ya 68 pasi ya Sharaf Shiboub.
Bao la tatu aliwatungua Biashara United, Septemba 29 kwa guu la kushoto asisti ya Ajibu dakika ya 55.
Bao la nne aliwatungua Singida United, Oktoba 27 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid dakika ya 42 kwa pasi ya Mzamiru Yassin alifunga kwa guu la kushoto aliwatungua Ruvu Shooting ilikuwa Novemba 23, dakika ya 39 kwa kichwa pasi ya Shomari Kapombe na bao la sita alifunga dakika ya 74 kwa guu la kulia
Huyu hapa ametengenezewa mabao
Kagere alitengenezewa asisti bao kwa Meddie Kagere mbele ya Biashara United pia alisababisha penalti mbili ndani ya ligi na zilifungwa na Kagere.
Ilikuwa mbele ya Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba wakati Simba ikishinda mabao 3-0 na Mbeya City Uwanja wa Uhuru wakati Simba ikishinda mabao 4-0.
Erasto Nyoni beki kiraka aliingia kwenye rekodi za kimataifa kwa kufunga bao moja kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Simba ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya UD Songo Uwanja wa Taifa.
Ni yeye Sheva alisababisha penalti wakati Simba ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems,’Uchebe’ ambaye ameshachimbishwa ilikuwa Agosti 25.
Bao la upande wa UD Songo lilijazwa kimiani na Luis Misqussone kwa adhabu ya faulo ila kwa sasa yupo ndani ya Simba.
Mechi alizocheza kwenye Ligi Kuu Bara ni tisa kati ya 28 ametumia dakika 508 uwanjani kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za misuli aliyoyapata mwaka jana kwenye timu ya Taifa ya Tanzania.
Mechi zake hizi hapa
Mechi zake alizocheza ilikuwa namna hii:-JKT Tanzania (30), Mtibwa Sugar (27) Kagera Sugar, (29), Biashara United (83), Azam FC (33), Singida United, (81), Mwadui (45), Mbeya City (90), Ruvu Shooting (90).
Spoti Xtra limefanya mahojiano na Sheva ambapo alifunguka namna hii:-
“Wakati wangu wa kuwa nje ya uwanja kuna vitu vigi nilikuwa ninakosa ila kwa kuwa sikuwa na namna ya kufanya ilibidi nifuate ushauri na maelekezo ya wataalamu.
Kipi ulikikosa?
“Mpira ni kazi yangu na mashabiki wangu walikosa kuona nikiwa ndani ya uwanja ila kwa sasa nimeanza kurejea kwenye ubora wangu nina amini mambo yatakuwa sawa.
Janga la Corona kwako unalitazamaje?
“Balaa kweli yaani mambo mengi yamebadilika kwa sasa kila mmoja hana amani, ninaamini tutapita salama katika wakati huu mgumu ambao tunapitia na maisha yataendelea.
Dakika chache uwanjani ila mambo makubwa kwa nini?
“Kuamini katika kile ambacho ninakifanya, kujituma na kupambana bila kukata tamaa. Kila mchezaji alikuwa ananipa ushirikiano hivyo name nina amini bado nina nafasi ya kufanya vizuri ligi itakaporejea kikubwa ni sapoti,” anamalizia Sheva