VIRUSI vya Corona ambavyo vinasababisha ugonjwa wa COVID-19 kwa sasa vimekuwa janga la dunia kwa kuibadilisha mambo na kufanya hali ya hofu itawale kila kona.
Kote hofu imetawala kuanzia kwa wachezaji, mashabiki mpaka makocha pia nao wanahofia janga hili hapa kuna kitu cha kujifunza kwamba tupo kwenye mapito magumu lazima tuikubali kwanza hali hii kisha mambo mengine yatafuata.
Serikali kwa kuligundua hilo ilichukua tahadhari mapema ambapo ilizuia mikusanyiko isiyo ya lazima na kuwataka watu kwa imani zao wasisahau kufanya ibada ikiwa na maana kwamba bado kuna nafasi ya kutoka kwenye janga hili iwapo wote tutaungana na kufanya ibada.
Katika hali ngumu ambayo wanafamilia wamichezo kwa sasa tunapitia ni lazima tukubali kwamba kimbilio letu ni Mungu pekee na ibada itatufanya tuwe salama wakati huu na wakati wote.
Aliyeziumba mbingu na nchi anajua maumivu ya watu wake ambao amewaumba na anatambua kwamba wote wanapata maumivu kutokana na janga hili ambalo linaleta hofu na balaa zito kwa dunia.
Tusisahau kwamba hata wachezaji nao wamekuwa wakifanya hivi mara kwa mara wanapoingia uwanjani kwa kufanya sala kwa imani zao na kuendelea na michezo jambo ambalo linamaanisha kwamba Mungu ni wetu sote.
Nimekuwa nikizungumza na makocha wengi bila kusahau wachezaji nao pia wamekuwa wakionyesha jambo la kipekee hasa wakati wa mahojiano wanaanza na Mungu kwanza kisha mengine yatafuata.
Ipo namna hii wakati huu tunaopita sio wa kuleta utani ni lazima kila mmoja apambane na kufuata tahadhari zote za kujikinga na virusi vya Corona.
Kusimama kwa Ligi Kuu Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi ya Wanawake pamoja na masuala yote yanayohusu michezo inafanya mambo mengi yasimame.
Matokeo yake yameanza kuonekana kwa wanafamilia za mpira ambapo wafanyabiashara kwa sasa wamekosa soko la bidhaa zao hasa wale waliokuwa wanamiliki vibanda umiza.
Achana na wajasiriamali ambao walikuwa wanategemea kuuza bidhaa zao ili wapate kipato wapo wale wengine ambao furaha yao kubwa ilikuwa kwenye soka na kuwaona wachezaji wakiwa uwanjani mambo yamekuwa magumu.
Kikubwa ambacho wapenda mpira kwa sasa tunatakiwa kukifanya ni kufuata kanuni za afya na kuendelea kufanya ibada bila kuchoka hili nalo litapita na kila kitu kitakuwa sawa.
Tukirudi kwa wachezaji ambao kwa sasa wao watakuwa kwenye mapumziko ambayo yanatarajiwa kukamilika Aprili 17 kwa sasa wanakuwa wapo huru kufanya mambo yao wanatakiwa kutobweteka na kuendelea kuishi bila kufanya mazoezi.
Kazi yao inakuwa ni moja tu kulinda vipaji vyao na kuendelea kuchukua tahadhari wakati wakifanya mazoezi ya kulinda vipaji vyao ili wabaki kuwa salama wao na familia zao pia.
Mashabiki pia wanapaswa kuwa na subira na kuendelea kufuata kanuni za afya huku wakiepuka mikusanyiko isiyo ya lazima kwa kufuata taratibu ambazo zimewekwa.
Imani yangu ni kwamba Mungu wetu ataskia maombi yetu na atajibu yale ambayo tunayahitaji sawasawa na mapenzi yake, Amen .
Post a Comment