BILIONEA na mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ ameweka hadharani kwamba wanamshusha kocha matata zaidi katika klabu hiyo ambaye ataziba pengo lote la aliyekuwa kocha wao Mbelgiji, Patrick Aussems.
Mo ametangaza kuwa wapo kwenye harakati za mwisho kabisa za kumleta kocha huyo ambapo keshokutwa Jumatano watamtambulisha kwa ajili ya kuanza kazi.
Simba kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kumshusha kocha mpya baada ya hivi karibuni kuvunja mkataba wa Aussems.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa mwaka wa Simba, Mo Dewji alisema kuwa anamleta kocha huyo ambaye atakuwa na kiwango cha kuifundisha timu hiyo kufikia malengo yao ya kutwaa ubingwa waliyojiwekea kwa msimu huu.
“Tunamleta kocha ambaye atakuwa na kiwango cha kustahili kuifundisha timu hii na kufikia malengo yake ambayo imejiwekea.
“Na kama kila kitu kitaenda sawa basi wiki hii Jumatano, tutamtambulisha kocha huyo kwa ajili ya kuja kuchukua nafasi ya kocha aliyepita.
“Tumekusudia kurekebisha eneo hilo na tunamleta kocha ambaye atatekeleza malengo yetu,” alisema Mo Dewji.
Hata hivyo, kumekuwa na usiri mkubwa juu ya kuletwa kwa kocha huyo ambaye atachukua mikoba ya Aussems ambapo kwa taarifa ambazo Championi Jumatatu, limezipata ni kuwa watu wawili pekee Mo mwenyewe na Mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa ndiyo wanamjua.
Wamarekani, Chambeshi, Gomez ndani
Katika hatua nyingine Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema kuwa hadi sasa wamepokea maombi ya makocha 72 ambao wameomba nafasi ya kuchukua mikoba ya Aussems ambamo miongoni mwao ni Kocha wa Nkana, Beston Chambeshi na Kocha wa Horoya AC, Paul Gomez pamoja na wengine kutoka Marekani na England.
“Tunaendelea na mchakato na Jumatano hii ndiyo kila mtu atajua nani kocha wetu mpya,” alisema Senzo
Post a Comment