BAADA ya uongozi wa Simba kumtambulisha Mbelgiji, Sven Vandenbroeck kuchukua nafasi ya Patrick Aussems, aliyekuwa kocha wa Nkana, Beston Chambeshi ameibuka na kusema hajui nini kilichotokea hadi kuachwa kwenye mataa kwa kuwa mazungumzo yao yalikwenda vizuri.
Vandenbroeck amechukua nafasi hiyo akiwapiga bao makocha wengine wawili ambao ni Frank Nuttall raia wa Scotland na Mzambia, Beston Chambeshi.
Simba ilimuita Chambeshi nchini na kuzungumza naye wiki iliyopita, baada ya hapo akarejea kwao alikodaiwa kwenda kuvunja mkataba wake uliobakia na Nkana kwa kuwa aliambiwa atarudi Dar kujiandaa kwa ajili ya kazi mpya.
Huku nyuma ikadaiwa kuwa Simba hawakufurahishwa na kocha huyo kuvujisha mpango wake wa kujiunga na timu hiyo kwenye vyombo vya habari, ndipo wakabadili maamuzi.
Alipotafutwa Chambeshi kutoka Kitwe, Zambia alisema: “Kiukweli sijui nini kimetokea maana wao waliniambia nisubiri tiketi ya ndege kwa ajili ya kuja huko kati ya Jumatatu na Jumanne kabla ya kuanza kazi lakini ikawa kimya muda wote walisema nisubirie.
“Sven amenipigia simu, amenieleza kuwa wamemchukua yeye, alishawahi kufanya kazi kwenye timu yetu ya taifa, tunajuana, siyo kitu kibaya huwa inatokea, japo bado nina ofa kutoka Rwanda na Afrika Kusini,” alisema Chambeshi.
Ibrahim Mussa, Dar es Salaam
Post a Comment