Katika kuelekea mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba, matajiri wa Yanga, Kampuni ya GSM ambao ndiyo wadhamini wa timu hiyo wamewalipa wachezaji wote wanaodai fedha za usajili. Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kabla ya wachezaji hao kulipwa stahiki zao, hivi karibuni GSM ilifanya balaa katika usajili kwa kusimamia usajili wa nyota kadhaa akiwemo Haruna Niyonzima.
Hiyo ikiwa ni siku chache mara baada ya wachezaji kulalamika kwenye mitandao ya kijamii wakidai kuwa hawathaminiwi kutokana na kutolipwa fedha zao za usajili kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, mabosi hao wamelipa stahiki hizo kwa wachezaji katika kuwapa morali kuelekea pambano lao dhidi ya Simba.
Mtoa taarifa aliwataja wachezaji hao waliolipwa stahiki zao ni Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Said Juma ‘Makapu’, Juma Abdul, Juma Mahadhi, Andrew Vincent ‘Dante’ na Ramadhani Kabwili.
Aliongeza kuwa, wachezaji hao wamelipwa madai yao juzi, huku wakipanga kuwalipa mishahara ya mwezi huu wa Desemba wiki hii hiyo o yote katika kutengeneza morali ya wachezaji.
“GSM wamepania kuifanyia makubwa timu katika kuelekea mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba, hivyo tayari jana (juzi) wamewalipa wachezaji wote waliokuwa wanadai fedha za usajili.
“Kati ya hao yupo Ngassa ambaye hivi karibuni alionekana kulalamika kwenye mitandao ya kijamii pamoja na Dante mwenyewe ambaye amerejea kikosini.
“Kikubwa GSM wanataka kuona hujuma na mipango wanayotaka kuwatumia wapinzani wao Simba hazifanikiwi na ndiyo maana wamewalipa wachezaji hao huku wakipanga kuwalipa mshahara wa mwezi huu wiki ijayo,” kilisema chanzo.
Alipotafutwa Ofi sa Habari wa Yanga, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo, alisema kuwa: “Hilo suala lipo kwa viongozi wa juu lakini kama umelipata basi itakuwa kweli, kwani viongozi hivi sasa wamepanga kufuta madeni yote ambayo tunadaiwa na wachezaji.”
Post a Comment