UONGOZI wa Klabu ya Yanga umetuma kikosi kazi nchini Uganda kumfuatilia straika wa timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Fahad Bayo kwa ajili ya kupata saini yake katika usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa wiki ijayo.
Hata hivyo, ukiachana na mchakato huo wa usajili unaoendelea kuna wachezaji wanne wa kimataifa kutoka Malawi, DR Congo na Eritrea, wametua kwa ajili ya kufanya majaribio kikosini hapo.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa kamati ya ufundi ya Yanga imetuma watu maalum katika michuano ya Cecafa kwa ajili ya kuangalia wachezaji wenye viwango ambapo tayari wameshafanikiwa kuanza mazungumzo na Fahad.
“Mchakato wa usajili unaendelea kama ulivyopangwa, kuna watu maalum ambao wameteuliwa kwa ajili ya kwenda kufuatilia michuano ya Cecafa kwa ajili ya kwenda kuangalia vipaji vya wachezaji katika michuano hiyo ili kupata nafasi ya kusajili wale ambao wataonekana wapo vizuri.
“Hadi sasa tayari kuna mshambuliaji wa Uganda, Fahad ambaye wajumbe waliokwenda kule wanafanya nae mazungumzo ya awali, hivyo mipango ikikamilika tutamsajili.
“Lengo letu ni kuboresha kikosi chetu katika nafasi ya mshambuliaji mmoja, viungo wawili, beki wa kushoto na beki wa kati mmoja, kuhusu wachezaji ambao tatawafungashia mikoba wapo, tunasubiria dirisha la usajili lifunguliwe ndipo tuweze kuwaweka wazi,” alisema Bumbuli.
Yanga inaonekana kuweka nguvu kusajili mshambuliaji kwa kuwa wamekuwa na tatizo la uhaba wa mabao katika michezo yao ya hivi karibuni, hivyo straika huyo anayeichezea Vipers S.C inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda anaonekana kuwa anaweza kutatua matatizo yao.
Khadija Mngwai, Dar es Salaam
Post a Comment