Katika kuhakikisha kiungo Haruna Niyonzima anauwahi mchezo dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, uongozi wa Yanga umepanga kumpandisha ndege mmoja wa viongozi kwenda nchini Rwanda kwa ajili ya kufuatilia Kibali cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) cha mchezaji huyo fundi.
Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana Januari 4, mwakani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mchezo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa timu hiyo. Niyonzima ni kati ya wachezaji wanaotarajiwa kuwepo katika mchezo huo baada ya kusajiliwa hivi karibuni na kupewa mkataba wa miaka miwili akitokea AS Kigali ya Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra, mabosi hao wamepanga kusafiri ndani ya wiki hii kwenda Rwanda kwa ajili ya kufuatilia kibali hicho kutoka kwenye Shirikisho la Soka la Rwanda (Ferwafa). Aliongeza kuwa viongozi hao wanaamini uwepo wa kiungo huyo
mwenye uwezo mkubwa wa kuchezesha timu na kupiga pasi za mwisho utakiimarisha kikosi chao kutokana na uzoefu alionao. “Viongozi wanataka kumuona Niyonzima akijiunga na kambi haraka mara baada ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Biashara United.
“Hivyo, mmoja wa viongozi atakwenda Rwanda kuhakikisha masuala ya ITC yake yanamalizika haraka kwani hiyo ndiyo inamchelewesha kuja nchini kujiunga na timu,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza kuwa. “Kiungo huyo tayari ameandaliwa nyumba atakayofikia kwenye ‘apatmenti’ za Shekilango alipokuwa anakaa aliyekuwa mshambuliaji wetu Urikhob (Sadney).
” Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alikazia ujio wa Niyonzima kwa kusema wanatarajia kumpokea hivi karibuni ili kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria. “Niyonzima ameomba kucheza mchezo wa mwisho na timu yake ya AS Kigali, kisha ndio afanye safari ya kuja Bongo tayari kwa ajili ya maandalizi ya mechi zinazofuata na uongozi umekubaliana naye. “Kuna vitu vichache tu ndivyo vilivyobaki kwa ajili ya kukamilisha usajili wake,” alisema Bumbuli. Wilbert Molandi na Khadija Mngwai,
Post a Comment