WAKATI uongozi wa Simba ukitarajiwa kuwatangaza wachezaji Bakari Mwamnyeto na Luis Jose Miquissone waliowasajili katika dirisha dogo, mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Ismail Rage ameufagilia usajili huo.
Rage amesema hana mashaka na usajili wa wachezaji hao kwani kikosi hicho kina upungufu ya wachezaji wawili katika eneo la ulinzi na safu ya ushambuliaji, baada ya mchezaji John Bocco kusumbuliwa na majeraha na kumfanya Meddie Kagere kuhitaji usaidizi.
“Simba ilikuwa na mahitaji ya wachezaji wawili, sina shaka na usajili wa Mwamnyeto kwani umbile lake ni kubwa, mrefu na ana nguvu za mwili hivyo anafaa kuimarisha safu ya ulinzi na Miquissone ni mzuri kwa mchezo mmoja niliomwona anafaa kumsaidia Kagere kwani John Bocco anaendelea kuuguza majeraha,” alisema Rage.
Simba inatarajia kumtangaza Mwamnyeto aliyekuwa Coastal Union na Miquissone mchezaji anayeichezea kwa mkopo timu ya UD Songo ya Msumbiji akitoka Mamelod Sundowns ya Afrika Kusini.
Miquissone mchezaji ambaye mashabiki wa Msimbazi hawawezi kumsahau kwani aliifunga bao kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya mabingwa Afrika na kufanya mchezo kumalizika kwa 1-1 na Simba kutoka kwenye michuano hiyo kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya mchezo wa awali kutoka suluhu.
Aidha Rage ametoa rai kwa benchi jipya la ufundi kumtumia beki ,Yusuf Mlipili ambaye amesugua benchi toka msimu umeanza na ni mchezaji mzuri ambaye ana uwezo kama ataaminiwa na kupewa nafasi atamsaidia Miraji Athumani na Simba itafika mbali.
“Nimeongea kwenye vyombo vya habari mara nyingi kuomba Simba kujaribu kutumia wachezaji chipukizi kwani wana uwezo, tumeona kwa Miraji ameonesha kitu cha tofauti anapaswa kuaminiwa pia Mlipili ni mzuri ana kitu ndani yake,” aliongeza Rage.
Alisema kama wanaona wachezaji zawa hawana nafasi ya kucheza katika kikosi hicho watafutiwe timu za kwenda ili kuwasaidia kulinda viwango vyao kwa sababu soka ndio kazi yao hivyo kutowapa nafasi inasababisha kukata tamaa ya kucheza angali bado vijana
Post a Comment