MABOSI Yanga wamekamilisha dili la usajili la mshambuliaji wa Azam FC anayekipiga kwa mkopo Polisi Tanzania Ditram Nchimbi wakitumia kitita cha Sh Mil. 40 kufanikisha usajili huo.

 

Yanga ni kama wamewazidi ujanja Simba baada ya kufanikisha usajili wa mshambuliaji huyo aliyekuwa anawaniwa na klabu hizo kongwe katika usajili huu wa dirisha dogo uliofunguliwa juzi Jumatatu.

 

Mshambuliaji huyo hivi sasa yupo nchini Uganda kwenye michuano ya Kombe la Cecafa, akiwa na kikosi cha Kilimanjaro Stars ambacho jana kilitarajiwa kujitupa uwanjani kucheza na Uganda kwenye Uwanja wa KCC.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano kutoka kwenye uongozi wa Azam, mshambuliaji huyo wamemuachia kwa dau hilo na kumtoa Polisi Tanzania alipokuwa anakipiga kwa mkopo.

 

Mtoa taarifa huyo alisema kati ya Sh Mil. 40, Azam imechukua Mil 20, huku mchezaji mwenyewe akichukua Mil 20 kama dau lake la usajili baada ya Yanga kuonekana kuvutiwa naye.

 

Aliongeza kuwa uongozi wa Yanga na Azam wamefikia makubaliano mazuri kwa pamoja kuvunja mkataba wake wa kuendelea kuichezea timu hiyo katika msimu huu.

 

“Nchimbi alionyesha nia kubwa ya kutaka kuondoka Azam ni baada ya yeye mwenyewe kuulazimisha uongozi ukubali kumuachia aondoke zake aende Yanga au timu nyingine lakini siyo kubakia hapo.

 

“Hivyo uongozi wa Azam haukutaka malumbano na mchezaji huyo na kufikia makubaliano ya pamoja kumuachia aondoke zake lakini kwa makubaliano ya kuuvunja mkataba kwa dau la Sh Mil. 20.

 

“Hivyo viongozi wa Yanga tayari wamesaini hundi ya Sh Mil. 20 na kuwapatia viongozi wa Azam huku ikibakia Mil. 20 ambazo hizo atapatiwa yeye kama dau lake la usajili,”alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla alikiri; “Leo au kesho (Jumatano) mwakilishi wetu kutoka Yanga atasafiri kwenda Uganda kwa ajili ya kwenda kumalizana na Nchimbi aliyepo kwenye kikosi cha Kilimanjaro Stars.”

Stori na Wilbert Molandi

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.