Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba, Sven Ludwig Vandenbroeck, licha ya kuomba siku 10 ili kukaa kwanza na timu hiyo kabla ya kuzungumza rasmi na vyombo vya habari nchini, amegusia kitu ambacho ni wazi atakuwa ameugusa 'mshipa wa fahamu' wa uongozi, wanachama na mashabiki wa
timu hiyo.

Baada ya kumtambulisha Jumatano usiku, uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kuwa jana kocha huyo angezungumza na waandishi wa habari, lakini baada ya wanahabari kuwasili eneo la tukio wakatangaziwa kuwa mkutano huo umeahirishwa na kwamba Sven ameomba apewe siku 10 za kukaa na wachezaji wake kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari.

Hata hivyo, mashabiki wengi na wadau wa soka baada ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 40, kutambulishwa Jumatano wiki hii, kupitia vyombo vya habari ikiwamo mitandao ya kijamii waliponda umri na mafanikio yake wakidai hataweza kuisaidia Simba kufikia malengo yake.

Kauli hiyo imeonekana kama imemfikia Sven, ambapo jana alikiri yeye ni kijana na kudai ataifundisha timu hiyo kisasa na baada ya muda mfupi wachezaji watakuwa wameshauzoea ufundishaji wake.

"Naomba nipewe muda kama wa siku kumi ndio nitaweza kuweka hadharani mikakati yangu kwa sababu bado sijakaa muda mrefu na timu, nikikaa nao ndio nitajua nini cha kuzungumza," alisema.

Hata hivyo, kupitia ukurasa rasmi wa Instagram wa klabu hiyo, kocha huyo alifunguka kwa kugusia jambo ambalo ni kama ameushika mshipa wa fahamu wa uongozi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo baada ya kueleza sehemu ya mikakati yake ambayo ndiyo kiu kubwa ya klabu hiyo.

“Lengo la kwanza ni kushinda ubingwa wa Ligi Kuu. Nataka kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, nataka kucheza mashindano ya CAF. Nataka Simba iwe kwenye hatua kubwa na kupata matokeo mazuri.

"Kilichonivutia Simba cha kwanza ni wingi wa mashabiki. Ni jambo la kufurahisha kuona mashabiki 60,000 wakikushangilia inakupa hisia za kipekee,” Sven alisema.

Sven jana aliendelea kukinoa kikosi hicho katika mazoezi yanayoendea kwenye Uwanja wao wa Simba Mo Arena, Bunju jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mwina Kaduguda alisema: "Kikao kilikuwa kifanywe leo [juzi] kocha azungumze na waandishi wa habari, lakini tumeahirisha tutakifanyika siku nyingine itakayopangwa," alisema Kaduguda.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.