Na Saleh Ally
MWEKEZAJI wa Simba, Mohamed Dewji, maarufu kama Mo, amesema maneno ambayo inawezekana kwa asilimia mia, viongozi wa soka na hasa kwa ngazi ya klabu, walipaswa kuwaeleza wachezaji wao mara kwa mara bila ya woga.


Wachezaji wa klabu kubwa nchini wamekuwa wakifanya mambo mengi sana katika mwenendo ambao si sahihi, mwenendo ambao hauendani kabisa na usahihi au weledi wa masuala ya mchezo wa soka hasa katika kile kiwango kinachoonekana kuwa kimepiga hatua.


Wengi wao wamekuwa wakienda kwa mfumo wa kizamani, wamelewa umaarufu na ukubwa walioupata kutokana na nguvu ya mashabiki wa klabu zao, wanautumia vibaya.
Mchezaji anachelewa katika mazoezi, anachelewa wakati wa kula na ikiwezekana anachelewa kwenye vikao na hakuna wa kumwambia.



Hofu ya kutomwambia ukweli au kumkemea inatokana na kwamba tayari mashabiki wanamkubali na wasingependa kuona anabugudhiwa. Mchezaji naye anaitumia hiyo kama nafasi ya kuendeleza kile ambacho si sahihi.


Hata waandishi ambao tumekuwa tukiwaeleza wachezaji wanaovurunda kuwa hawako sawa na wanapaswa kuweka nguvu nyingi katika nidhamu, pia tumekuwa tukionekana ni maadui.


Viongozi nao wanaweza kuongoza katika hilo hata kama wanajua unawasaidia. Lakini kwa kuwa kila kiongozi anataka aonekane ni malaika kwa mashabiki na wanachama, yuko tayari kutetea kila aina ya uozo.


Kuwafanya wanachama na mashabiki wawe na furaha ndio yamekuwa malengo ya viongozi wengi wa klabu hizi kubwa. Ndio maana wengi wao wamekubali kujawa na unafiki, uzandiki na uzabizabina bila hata ya woga kwa kuwa kichaga chao kimekuwa ni mashabiki na wanachama.


Ukisikiliza kauli ya Mo Dewji, inaonyesha weledi, mabadiliko makubwa na kiwango cha juu cha weledi, kusema ukweli bila ya woga na kuwa na malengo ya kusaidia taasisi badala ya mtu mmojammoja au mtu binafsi pekee.


Viongozi kwa muda mwingi sana, wamekuwa wakitetea maslahi yao na si taasisi. Kauli ya Mo Dewji utofauti wake unaonyesha ni malengo kwa ajili ya taasisi. Kuwa taasisi ni kubwa kuliko yeyote aliyemo ndani. Ninaamini Mo Dewji anatambua Simba ni kubwa kuliko yeye au mwingine yeyote aliye ndani yake ndio maana amesema kauli hiyo ambayo inatolewa na kiongozi mwenye nia njema na klabu kwa manufaa ya miaka na si furaha ya muda ya mashabiki na wanachama.


Wako mashabiki na wanachama lakini baadhi ya viongozi hawapendi hata wachezaji wanaolalamikiwa kwa utovu wa nidhamu kama Jonas Mkude kuambiwa ukweli.


Unaweza kuona ukishambuliwa kwa maneno ya lawama, eti unamchanganya Mkude kwa kumueleza abadilike. Tena utasikia unamchanganya kwa kuwa umejua tuna mechi ngumu, “umetumika”.


Kauli hizi za kipuuzi hazinipi shida mtu kama mimi. Wako ambao wameamua kuacha kusema ukweli kwa hofu ya kushambuliwa kwa maneno, jambo ambalo siwezi kulifanya.
Leo pamoja na kusema kwa ajili ya wote lakini ujumbe wa Mo Dewji utakuwa umemfikia Mkude na wengine wote wenye tabia kama zake. Kwamba ni lazima wabadilike, wafanye kazi kwa ajili ya taasisi na nidhamu ndio jambo namba moja.


Dewji amesema nidhamu ni namba moja na hata mafanikio yake yametokana na nidhamu. Itakuwa poa kasema Mo Dewji, huenda wale ambao walikuwa wakipinga wakati tukilisisitiza hilo, safari hii wataelewa kutokana na aliyosema.


Hakuna ambaye amewahi kufanikiwa bila ya nidhamu. Cristiano Ronaldo na Lionel Messi pamoja na mafanikio mlima, bado wana nidhamu ya juu kabisa. Vipi iwe kwa Mkude au wachezaji wa kigeni kama Clatous Chama na Sharaf Shiboub ambao unatarajia kuona matunda kwa kiwango cha juu lakini sasa nao wanaonekana kuwa “wamelivamia” jiji!


Kila mtu ana haki ya kustarehe, lakini lazima kufanya kilicho sahihi kwa yule anayekulipa vizuri kwani anafanya hivyo ili kupata matunda bora. Mo Dewji pia kalisisitiza hili na huu utakuwa ujumbe kwa wachezaji wote pia.
Ameelezea machungu ya nidhamu na iko wazi, huna nidhamu unaanguka. Lazima uwe na nidhamu ili kutengeneza usahihi wa mambo.


Hivyo, kuweni wakweli na achaneni na kufuga matatizo yanayozitafuna klabu hizi kubwa kwa miaka nenda rudi kwa ajili ya furaha ya muda mchache.


Wanaosema ukweli, mtafakari wanachokisema kabla ya kuanza kuwashambulia bila ya kujua ukweli.


Simba haiwezi kuwa na mafanikio kama hakuna nidhamu. Hata kuwe na fedha namna gani, kama hakuna nidhamu, mafanikio yakipatikana yatakuwa ni ya muda mfupi sana. Ninaamini Simba haitaki mafanikio ya muda mfupi.
Suala la nidhamu ndani ya timu kubwa liko chini.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.