Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Adolf Rishard, amefunguka juu ya sakata la usajili wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Cleophace Mkandala, kuhusishwa kutakiwa na Klabu ya Yanga kwa kusema mchezaji akikubali yeye kwake hana tatizo.
Mkandala aliwahi kucheza katika timu ya vijana ya Yanga kabla ya kutimkia mkoani Mbeya ambapo alienda kujiunga na Tanzania Prisons, kiungo huyo aliingizwa kwenye rada za Yanga baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika Ligi Kuu Bara msimu huu hususan katika mechi dhidi ya Simba iliyoisha kwa sare ya bila kufungana.
Inaelezwa kuwa, Yanga ilikuwa ikimsubiri mchezaji huyo arejee kutoka katika Michuano ya Cecafa inayofanyika nchini Uganda ili waweze kukamilisha usajili wa mchezaji huyo ambaye amebakisha mkataba wa miezi sita katika kikosi cha Prisons.
“Hata mimi nimesikia hizo tetesi lakini bado sijapata taarifa rasmi kutoka kwenye uongozi wa klabu, lakini Mkandala bado ni mchezaji wetu na yupo katika mipango yetu ingawa nikipata taarifa lazima nitatoa ushirikiano kwenye maongezi juu ya suala hilo kama mkuu wa benchi la ufundi, nitampa ushauri na akionyesha kuwa tayari nitamruhusu,” alisema Rishard.
Hata hivyo, Kocha huyo alithibitisha kuwa kwa sasa wana mpango wa kufanya usajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao huku akisisitiza kuwa tayari kuna baadhi ya wachezaji ambao wamewafuatilia na wanafanya nao mazungumzo ili waweze kumalizana nao katika dirisha hili dogo la usajili.
“Ni kweli hata sisi tunataka kusajili kipindi hiki na kwa sasa hivi kuna wachezaji ambao tumewaangalia ingawa bado tupo kwenye mazungumzo nao, kwa sababu bado wapo katika mazungumzo na klabu nyingine lakini mpango huo tunao,” alisema kocha huyo
Post a Comment