Kamati ya Ufundi na Mashindano ya Yanga imesema kuwa wapo tayari wawaachie wachezaji wao wote wa kimataifa waondoke lakini siyo mshambuliaji Mkongomani, David Molinga na Mghana, Lamine Moro.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu wapate taarifa za wachezaji wao sita wa kimataifa kutangaza kuvunja mikataba yao na kujipanga kurudi nyumbani kwao kwa kile kilichotajwa madai ya malipo ya mishahara ya miezi miwili.
Wachezaji hao ni Issa Bigirimana, Juma Balinya, Maybin Kalengo, Sadney Urikhob, Molinga na Lamine ambao wote walisajiliwa kwenye msimu huu wa ligi.
Kwa muijibu wa kikao kilichokaa jana cha Kamati ya Ufundi na Mashindano ya timu hiyo, kwa pamoja wameridhia wachezaji hao kuondoka huku wakiweka mikakati ya kuhakikisha wanawabakisha Molinga na Lamine kwa kuwalipa madai yao ili warejee kikosini.
Mtoa taarifa huyo alisema wachezaji hao wengine wanawaachia kutokana na kutokuwa na mchango katika michezo ya Ligi Kuu Bara na mashindano ya kimataifa waliyokuwa wanashiriki.
Aliongeza kuwa tayari uongozi umeanza kufanya jitihada hizo za kuwarejesha kikosini nyota hao wawili licha ya kuandika barua za kusitisha mikataba yao.
“Ni ngumu kwa viongozi, pia kaimu kocha wetu Mkwasa (Charles) kukubali kumuachia Molinga na Lamine kutokana na mchango mkubwa walioutoa kwenye timu katika michezo ya ligi.
“Hivyo viongozi wamekutana leo (jana) haraka kwa ajili ya kukamilisha mipango hiyo ya kuwarejesha kikosini wachezaji hao kwa kuwalipa stahiki zao za mishahara na posho wanazodai.
“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa wachezaji hao wawili tukielekea kwenye mchezo wetu wa ligi dhidi ya Simba, hivyo ni lazima warejee kikosini, lakini hao wengine tupo tayari kumalizana nao kwa kuwaacha waondoke zao,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Hassani Bumbuli kuzungumzia hilo alisema: “Hilo suala lipo kwenye Kamati ya Utendaji na siyo kwangu, hivyo likifika kwangu nitalizungumzia.”
Post a Comment