LABDA Seleman Matola amnyime tu jezi, lakini madaktari wa Afrika Kusini wamewaambia Simba kwamba, John Bocco ruksa kurejea uwanjani dhidi ya Yanga, Januari 4.
Simba watacheza na Yanga mchezo utakaopigwa Januari 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa huku kwenye benchi la Jangwani akitarajiwa kuwemo Charles Mkwasa na Kally Ongala au Mecky Maxime pembeni.
Bocco anarejea uwanjani baada ya kukaa nje muda mrefu akiuguza maumivu ya misuli yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu huku akiikosa michezo yote ya ligi waliyocheza.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra na kuthibitishwa na Daktari Mkuu wa timu hiyo, Yassin Gembe kuwa mshambuliaji huyo amerejea kutoka Sauzi alipokwenda kufanyiwa vipimo vya mwisho baada ya kumaliza matibabu ya hapa nchini.
“Bocco tayari amerejea nchini akitokea Sauzi alipokwenda katika vipimo vya mwisho baada ya kumaliza matibabu ya madaktari wa timu aiyokuwa akiyafanya kwa kipindi kirefu.
“Hivyo, hivi sasa anaendelea vizuri na mapema Januari, 2020 atakuwa fiti kwa asilimia mia moja, hivyo mashabiki wa Simba watarajie kumuona Bocco akirejea kwa nguvu zote katika timu,” alisema Gembe.
Kurejea Kwa Bocco kutaimarisha kikosi hicho kwenye safu ya ushambuliaji baada ya muda mrefu kumtegemea mshambuliaji mmoja Mnyarwanda, Meddie Kagere ingawa Miraji Athuman nae amekuwa moto wa kuotea mbali kwa siku za karibuni.
WILBERT MOLANDI, Dar
Post a Comment