YANGA ina majina mawili ya Makocha mezani ambayo mmoja wao ndiye atakayekuwa kocha msaidizi wa Yanga kuanzia mwezi ujao na wote ni vijana machachari.
Ingawa bado mchakato wa kocha mkuu unaenda taratibu lakini Yanga wako kwenye mjadala mzito wa yupi wampitishe kama msaidizi kati ya Kally Ongala na Mecky Maxime ambaye kwa sasa yuko na Kagera Sugar.
Ongala ambaye ni raia wa Uingereza aliyekulia Sinza, amewahi kuichezea na kuifundisha Azam kwa vipindi tofauti huku Yanga wakiamini kwamba ana mapenzi makubwa na timu yao.
Spoti Xtra limejiridhisha kuwa, hatma ya kocha msaidizi itajulikana wikiendi hii itakapokutana Kamati ya Ufundi chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Charles Mkwasa.
Lakini Yanga wamepanga kumpa Mkwasa nafasi ya kukaimu mpaka baadaye mwakani watakapoleta kocha mkuu lakini mchakato wa kina Ongala na Maxime unatakiwa kumalizika mapema.
Alipotafutwa Maxime kuzungumzia hilo alisema kuwa “Nipo tayari kutua Yanga muda wowote hata hivi sasa, kikubwa ni tukubaliane maslahi tu ya kazi yatakayonishawishi mimi kufanya kazi nao.
“Kwa sasa nipo Morogoro nimepumzika, hivyo kama wananitaka, ni tayari hata leo wao wanitumie nauli, haraka nitakuja huko Dar kwa ajili ya kumalizana nao,” alisema Maxime ambaye alistaafu Taifa Stars kwa heshima.
NIYONZIMA Wikiendi hii mabosi wa Yanga watakuwepo nchini Rwanda wakimuangalia kwa jicho la pili kiungo fundi Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ ambaye wanafikiria kumrejesha kikosini mwezi huu.
Yanga ipo katika mipango ya kuboresha sehemu mbili ambazo ni ushambuliaji na kiungo mchezeshaji katika usajili wa dirisha dogo utakaofunguliwa Desemba 16, mwaka huu na tayari mapendekezo yametolewa ya usajili huo.
Mtoa taarifa huyo alisema mabosi wawili kutoka Kamati ya Ufundi ya Yanga wikiendi hii watakuwepo nchini Rwanda kwa ajili ya kumuangalia Niyonzima atakayekuwa uwanjani akicheza mchezo wao wa ligi kuu akiwa na timu yake ya AS Kigali.
Aliongeza kuwa lengo la kwenda kumuangalia kiungo huyo ni kwa ajili ya kujiridhisha uwezo wake ule aliokuwa nao bado anao na wakiridhishwa naye haraka watampa mkataba ili ajiunge na timu hiyo kabla ya kukutana na watani wao Januari 4, mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Post a Comment