BAADA ya kukaa Manchester United kwa takribani miaka miwili, hatimaye jana Jumatano, Jose Mourinho alirejea klabuni hapo.
Mourinho alirejea na kikosi cha Tottenham Hotspur maarufu Spurs kilichokwenda kucheza dhidi ya Manchester United kwenye Uwanja wa Old Trafford ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu England.
Kocha huyo raia wa Ureno ambaye aliinoa Man United kuanzia 2016 hadi 2018 alipotimuliwa, alishuhudia kikosi chake kikianza kufungwa na Marcus Rashford dakika ya sita tangu kuanza kwa mchezo huo.
Dakika ya 25, ilibaki kidogo Rashford aongeze bao la pili, lakini shuti lake la umbali wa mita 35, liligonga mwamba wa juu na kurudi mchezoni huku mlinda mlango wa Spurs, Paulo Gazzaniga akifanya kazi ya ziada kuugusa kidogo mpira huo usiingie langoni.
Spurs ikaamka baada ya kushambuliwa mara kwa mara na dakika ya 39, Dele Alli, akaisawazishia timu yake bao ambalo lilikuja kuthibitishwa na VAR baada ya kuonekana kulikuwa na dalili za mfungaji huyo kuushika mpira kabla hajafunga.
Timu zikaenda mapumziko zikiwa sare ya bao 1-1 huku kila moja ikijitahidi kumshambulia mwenzake.
Dakika tatu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Rashford akaiongezea Man United bao la pili kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa na Moussa Sissoko kwenye eneo la hatari.
Hadi mwamuzi wa mchezo huo, Paul Tierney anapuliza filimbi ya mwisho, matokeo yalikuwa ni Man United 2-1 Spurs.
Hiki kinakuwa ni kipigo cha kwanza kwa Mourinho tangu aanze kuinoa timu hiyo akichukua mikoba ya Mauricio Pochettino. Mourinho ameiongoza Spurs katika mechi nne, ameshinda tatu na kufungwa moja.
Matokeo ya mechi zingine za Premier zilizochezwa jana ni; Chelsea 2-1 Aston Villa, Leicester City 2-0 Watford, Southampton 2-1 Norwich City, Wolverhampton 2-0 West Ham na hadi tunakwenda mitamboni, Liverpool ilikuwa mbele kwa mabao 4-2 dhidi ya Everton.
MANCHESTER, England
Post a Comment