Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya dirisha dogo kufunguliwa, uongozi wa Yanga umeamua kufanya kweli kwa muuaji wa Simba, Gerald Mdamu anayekipiga Mwadui FC kwa kumtumia tiketi ya gari lenye hadhi ya daraja la kwanza kutua Bongo.
Mdamu anayekipiga Mwadui FC ni kinara wa kutupia mabao klabuni hapo, akiwa nayo manne mpaka sasa. Alikuwa mchezaji wa kwanza kuiua Simba iliyokuwa haijafungwa mechi sita za ligi msimu huu, mchezo uliochezwa Kambarage na Mwadui ilishinda bao 1-0.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa Mdamu zilieleza kuwa tayari Mdamu kwa sasa yupo Bongo akifanya mazungumzo na mabosi wa Yanga ambao wanahitaji kuongeza nguvu ya kikosi kuelekea kwenye mchezo wao dhidi ya Simba.
“Kwa sasa Mdamu yupo Bongo na ameletwa na watu ambao ni vigogo wa Yanga na walimtumia tiketi ya gari lenye hadhi ya daraja la kwanza hivyo kwa sasa chochote kinaweza kutokea,” alieleza mtoa taarifa.
Championi Jumatatu lilizungumza na Mdamu ambaye alisema kuwa ni kweli yupo Bongo ila amekuja kwa ajili ya masuala yake binafsi.
“Nipo Bongo kweli siwezi kukuficha ila nimekuja kwa mambo yangu binafsi muda si mrefu nitarejea Mwadui kwa ajili ya kuendelea na maandalizi ya ligi,” alisema Mdamu.
David Chakala, Meneja wa Mwadui FC alisema kuwa kwa sasa hawajapata taarifa kuhusu mchezaji wake kuhitajika na Yanga, hivyo wakati ukifika watalizungumzia.
Championi Jumatatu lilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela azungumzie ishu hiyo lakini simu yake ilikuwa haipokelewi.
Post a Comment