BAADA ya aliyekuwa kocha wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems kubeba mabegi yake na kusepa kwao, uongozi wa timu hiyo fasta, umemshusha Mzambia, Beston Chambeshi.
Aussems aliondoka juzi usiku baada ya kumalizana na viongozi wa timu hiyo kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake kwa madai ya utovu wa nidhamu na kushuka kiwango kwa timu hiyo.
Lakini wakati kocha huyo akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa ajili ya kuondoka wakati huohuo, Simba wakatumia mlango wa kupokelea wageni kwa kumpokea Chambeshi anayefundisha Nkana inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia.
Licha ya Simba kufanya siri juu ya ujio wa kocha huyo lakini Championi Ijumaa lilifahamu kila kitu juu ya ujio wake akiwa amefichwa katika moja ya hoteli za kitalii jijini Dar.
Inadaiwa kuwa kocha huyo jana alitakiwa kukutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ lakini haikuwezekana kwa kuwa kiongozi huyo bado hajarejea nchini kwa kuwa bado yupo nje ya nchi, akitarajiwa kuwasili leo Ijumaa.
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na kocha huyo moja kwa moja kwa njia ya simu baada ya kupata namba yake kutoka kwa mtu wake wa karibu wa Zambia.
Kwanza alikiri kuwa yupo Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumza na uongozi wa Simba.
“Kweli nipo Dar es Salaam nimeitwa na Simba lakini nani amekueleza wewe kama nipo Dar?
“Sina cha kusema kwa sasa kwa kuwa wamenieleza leo mchana (jana) tutaenda kufanya mazungumzo ya kuona tunakubaliana nini baada ya hapo ndiyo nitakutafuta kukueleza tulichofikia,” alisema Chembeshi.
Alipoulizwa kikao hicho kitafanyika wakati gani alishindwa kuweka wazi kwa kusisitiza atafafanua baada ya kikao hicho huku pia akigoma kutaja hoteli aliyokuwa amefikia.
Alipotafutwa mtoto wa kiume wa kocha huyo, anayefahamika kwa jina la Junior Chambeshi alisema:
“Ni kweli baba amekwenda Tanzania kwa ajili ya kufanya ununuzi wa magari baada ya kupata muda wa mapumziko kutokana na kumalizika kwa michuano ya Vijana ya Kombe la Mataifa Afrika U-23 iliofanyika Misri.”
Kauli hiyo inathibitisha ujio wa kocha huyo ndani ya Simba kutokana na kufanana kwa taarifa na aliyekuwa kocha wa Yanga, Mzambia George Lwandamina wakati alipokuja nchini kumalizana na Yanga, alidai kuwa amekuja kununua magari kabla ya siku chache kutambulishwa.
Chambeshi aliyewahi kufanya kazi na kiungo wa Simba, Mzambia, Clautos Chama akiwa na Klabu ya Power Dynamo, timu ya taifa ya vijana ya Zambia nchini ya 20 na Nkana, ambayo yupo nayo kwa sasa anatarajia kumalizana na uongozi wa Simba kabla ya kesho Jumamosi watakapokuwa wakizindua Uwanja wa Bunju Complex kwa kuwa Jumatatu ataanza maandalizi rasmi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga.
Baadaye kocha huyo alitoa ushirikiano kwa kusema kuwa hawakufanikiwa kuzungumza na viongozi wa Simba kwa juzi.
CHANZO: CHAMPIONI
Post a Comment