Mabosi wa Polisi Tanzania, wamefungua njia kwa timu ya Yanga ambayo inaelezwa kuwa inahitaji saini ya nyota wao Ditram Nchimbi anayekipiga hapo kwa mkopo akitokea Azam FC.
Nchimbi ametupia jumla ya mabao manne ndani ya ligi alikuwa ni mchezaji wa kwanza kusepa na mpira baada ya kuifunga hat-trick Yanga Uwanja wa Uhuru na alitimiza majukumu yake ndani ya Stars kwa kufunga bao la ushindi mbele ya Sudan na kuifanya Stars kukata tiketi kushiriki michuano ya Chan nchini Cameroon 2020.
Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema; “Usajili haupo kwenye mitandao ama maneno matupu kwani kusikia kwamba wanamhitaji Nchimbi hilo nimeliskia ila bado hawajafika nina amini wakija tutazungumza kwani mchezaji kazi yake ni kucheza.
“Ila wanapaswa watambue kwamba Nchimbi yupo hapa kwa mkopo ni lazima pia wawasiliane na mabosi wao ambao ni Azam kisha sisi tutajua namna ya kufanya kwani wachezaji wapo wengi na dirisha la usajili linakaribia kufunguliwa,” alisema Lukwaro.
Dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Desemba 16 mwaka huu huku Yanga iliyo chini ya Boniface Mkwasa ikitajwa kuiwinda saini ya nyota huyo aliyecheza Njombe Mji ambayo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Post a Comment