Jose Mourinho ameteuliwa kuwa mkufunzi mpya wa Tottenham akichukua mahala pake Mauricio Pochettino ambaye alifutwa kazi siku ya Jumanne
Aliyekuwa mkufunzi wa Man United na Chelsea Mourinho ametia saini kandarasi hadi mwisho wa msimu wa 2022-23.
''Jose ni mmojawapo wa wakufunzi waliofanikiwa sana katuka soka'', alisema mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy.
Jose Mourinho alidaiwa kuwa katika mazungumzo ya kuchukua mahala pake Mauricio Pochettino kama mkufunzi wa Tottenham.
Pochettino mwenye umri wa miaka 47 alifutwa kazi kama mkufunzi wa Spurs siku ya Jumanne baada ya kuhudumu katika klabu hiyo kwa kipindi cha miaka mitano akiisimamia klabu hiyo ya kaskazini mwa London.
Raia huyo wa Argentina aliiongoza Spurs katika fainali ya kombe la klabu bingwa Ulaya msimu uliopita ambapo walipoteza kwa Liverpool.
- Mourinho afutwa kazi Manchester United
- Guardiola 'ametukosea heshima'- Pochettino
- Mourinho: Imekuwa vigumu kuwakimbiza Man City
Mourinho ambaye ni raia wa Ureno amekuwa bila kazi ya ukufunzi tangu alipofutwa kazi na United mnamo Disemba 2018.
Kumekuwa na ripoti kuhusu mkwaruzano kati ya Pochettino na mwenyekiti wa klabu hiyo Daniel Levy , lakini uamuzi huo ulichukuliwa kutokana na msururu wa matokeo mabaya katika kipindi cha miezi kadhaa , kuanzia Februari iliopita.
Mkufunzi wa Bournemouth Eddie Howe, kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsmann na aliyekuwa kocha wa Juventus Masimilliano Allegri wote wamehusishwa na uhamisho wa kujiunga na Spurs.
Hatahivyo Mourinho anajiandaa kuchukua ukufunzi wa klabu hiyo na iwapo mazungumzo kati yake na klabu hiyo yatakamilika vyema , tangazo linaweza kutolewa mapema siku ya Jumatano asubuhi muda wa London.
Baadhi ya maafisa katika klabu hiyo wanaendelea kuwa na matumaini kwamba Mourinho huenda akazinduliwa katika mkutano na vyombo vya habari siku ya Alhamisi iwapo mazungumzo yatakamilika vizuri.
Uchambuzi
Spurs haijawahi kumsajili mkufunzi aliye na mahitaji ya kiwango cha juu zaidi kama Mourinho , na wala haijawahi kutumia fedha nyingi kuwanunua wachezaji kama vile alivyozoea katika klabu za Real Madrid na Man United.
Hivyobasi mashabiki wengi watashangazwa kwamba huenda akajiunga na klabu hiyo huku kocha wa RB Leipzig Julian Nagelsman akionekana kijana zaidi na mwenye uwezo wa kuongoza klabu hiyo.
Lakini Spurs katika miaka ya hivi karibuni wametoka mbali chini ya ukufunzi wa Pochettino .
Wana uwanja mpya uliojengwa kwa thamani ya pauni bilioni moja na uwanja wa mazoezi mbali na kufuzu kushiriki katika ligi ya mabingwa mara nne mfululizo huku uuzaji wa baadhi ya wachezaji ukiwasaidia na kuifanya klabu kuwa klabu iliojipatia faida kubwa duniani.
Kwa sasa wana kikosi chenye talanta.
Mourinho amekuwa nje ya ukufunzi kwa takriban mwaka mmoja sasa na huku akiendelea kuishi mjini London, kazi hiyo inamfaa sana.
Post a Comment