Baada ya kutoweka kwa siku mbili Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems alirejea nchini na kuwataka wachezaji wake kufunga mabao ya mashuti kwa umbali wa mita 20 katika mazoezi, lakini straika wake, John Bocco ndiye ambaye alikuwa hatari katika mipango hiyo mipya.
Kocha huyo aliyeipa Simba mafanikio katika msimu uliopita kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kucheza robo fainali, alitumia mpango huo wa mashuti kwenye mazoezi yaliyofanyika jana Alhamisi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Simba imetumia mbinu hiyo katika mazoezi hayo ya kujiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting unaotarajiwa kupigwa kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar.
Gazeti la Championi ambalo lilikuwepo uwanjani hapo, lilimshuhudia kocha huyo akitumia zoezi la pembe tatu kwa kuwataka wachezaji wote kuhakikisha wanapiga mashuti golini kwa mipira ya kutengeneza nafasi ikiwa nje ya mita 18.
Bocco ambaye alikuwa nje ya uwanja muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi, alionekana kuwa moto wa kuotea mbali kutokana na kufanikiwa kufunga mabao matano katika mashuti sita yaliyolenga golini tofauti na wachezaji wengine ambao hawakuvuka mabao manne.
Hata hivyo, Bocco aliyekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya kifundo cha mguu alionekana kutumia mguu wa kushoto kupiga mashuti badala ya mguu wa kulia ambao amekuwa akiutumia mara nyingi kutokana na kupewa programu maalum na daktari wa timu hiyo, Yassin Gembe.
Kabla ya hapo Bocco ambaye kukosekana kwake kulisababisha pengo hasa kwa kuwa Simba ilimtegemea zaidi Meddie Kagere katika ufungaji, alisema: “Kitu kibaya ni kwamba hadi sasa mimi na Kagere hatujacheza sambamba pamoja tukiwa wawili.
Tulicheza msimu uliopita lakini tulikuwa watatu mimi, Kagere na Okwi kwa hiyo ikatunyima nafasi ya kucheza sambamba. “Niseme tu wazi kuwa naona kabisa tutasumbua wakati ambao tutacheza pamoja.”
Msimu uliopita Bocco na Kagere walifunga mabao 39 katika Ligi Kuu Bara, Kagere alifunga 23 akiwa ndiye mfungaji bora na Bocco akifunga 16
Post a Comment