MASHABIKI wa Klabu ya Real Madrid juzi walimzomea mshambuliaji wao Gareth Bale, kuanzia akiwa kwenye benchi kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) dhidi ya Real Sociedad.
Katika mchezo huo ambao Madrid waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, mashabiki hao walianza kumzomea mshambuliaji huyo kuanzia akiwa anapasha misuli moto, akiwa kwenye benchi na hata alipoingia uwanjani.
Hili limetokea kutokana na bango ambalo Bale alitumia kushangilia kwenye timu yake ya Taifa ya Wales ambayo ilipata nafasi ya kufuzu Euro 2020.
Bale alibeba bango lililokuwa na maandishi ya “Wales, Golf, Madrid”, akiwa anamaanisha kuwa kipaumbele cha kwanza kwake ni kuichezea Wales, pili kucheza gofu na tatu ndiyo kuitumikia Madrid.
Tukio hilo limeonyesha kuwakera mashabiki hao kwa kuwa wanaamini alionyesha dharau kwa klabu yao.
“Sidhani kama hali hii itaendelea msimu mzima, naona kuwa ni jambo la muda mfupi na litamalizika hivi karibuni na kila kitu kitakwenda vizuri,” alisema kocha wa Madrid, Zinedine Zidane.
Katika mchezo huo Madrid walifanikiwa kujipatia mabao yao kupitia kwa Karim Benzema ambaye alifunga bao lake la kumi kwa msimu huu, Luka Modric na Federico Valverde
Post a Comment