KATIKA kuhakikisha wanapata pointi tatu, mabosi wa Yanga watano, leo alfajiri walitarajiwa kusafiriki kwa ndege kutoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza kwa ajili ya kuiongezea hamasa timu yao itakapokuwa uwanjani ikivaana na Alliance School ya mkoani huko.
Timu hizo zitavaana katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa baada ya juzi Alliance kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa Azam FC.
Yanga kwenye mchezo huo inatarajiwa kuwakosa wachezaji wake muhimu watano kati ya hao wanne wapo kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Zanzibar Heroes ambao ni Issa Mohamed ‘Banka’ Abdulaziz Makame, Ali Ali na Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku Mapinduzi Balama naye akisumbuliwa na maumivu ya nyonga.
Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema lengo la viongozi kusafiri kwenda mkoani huko ni kwa ajili ya kuongeza hamasa ya wachezaji na mashabiki kujitokeza kwa wingi ili kufanikisha wanapata pointi tatu zitakazowaweka katika nafasi nzuri kwenye msimamo.
Nugaz alisema kuelekea mchezo huo utakaopigwa saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza wadhamini wa timu hiyo ambao ni wauzaji wa jezi, GSM wametenga tena kitita cha Sh milioni 10 kama timu ikipata ushindi, ikiwa ni sehemu ya kuwaongezea morali kwa wachezaji wao.
Aliwataja viongozi waliotarajiwa kusafiri kuwa ni Mkurugenzi wa Mashindano, Thabithy Kandorro, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi Salum Rupia, Katibu Mkuu David Ruhango, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Rogers Gumbo na yeye mwenyewe. “Kila kitu kinakwenda vizuri katika kuelekea mchezo huo ambao tumepanga kuchukua pointi tatu muhimu zitakazotuwezesha kupanda juu kwenye msimamo wa ligi ambayo ndiyo malengo yetu.
“Tunataka kuona mashabiki wengi wakijitokeza uwanjani kuwasapoti vijana wetu, wakiendelea kupata sapoti hiyo, pia siku hiyo kabla ya pambano asubuhi tutakwenda kutoa misaada Hospitali ya Bugando ya palepale Mwanza kwenye wodi ya mama wajawazito na watoto kwa kutoa magodoro 200, sukari kilo 200 na mataulo 200,” alisema Nugaz.
Mkwasa abadili program Katika hatua nyingine kikosi cha timu hiyo jana asubuhi na jioni kilifanya mazoezi mara mbili tofauti na ilivyokuwa progam yao ya kawaida, katika kujiandaa na mchezo huo chini ya Kaimu Kocha Mkuu Charles Boniface Mkwasa, yaliyofanyika asubuhi Uwanja wa Butimba na jioni Uwanja wa CCM Kirumba utakaotumika kuchezea mechi.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo Mkwasa alisema kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu kutokana na wapinzani wao kutopata matokeo mazuri katika mchezo wao uliopita. “Siwezi kueleza mipango kwa undani ila tumejipanga kushinda, tunajua tutapata changamoto kwa sababu wapinzani kupata matokeo yasiyoridhisha kwenye mechi yao iliyopita, ishu ya uwanja hainipi wasiwasi naujua vizuri,” alisema Mkwasa.
Post a Comment