BAADA ya straika wa Paris Saint Germain, Edinson Cavani kuhusishwa kutua La Galaxy ya Ligi Kuu Marekani, wakala wa mchezaji huyo, Walter Guglielmone amefunguka kuwa bado staa huyo ana uwezo wa kucheza kwa kiwango cha juu katika ligi kubwa za Ulaya.
Cavani ambaye ni mfungaji bora wa wakati wote ndani ya PSG, msimu huu hajauanza vyema na hii ni kutokana na kuwa nje kwa muda mrefu akiuguza majeraha. Amecheza mechi sita tu.
Hivi karibuni amekuwa akihusihwa na timu kadhaa na ikidaiwa kuwa PSG haina mpango wa kumuongezea mkataba kutokana na uwepo wa Mauro Icardi ambaye yupo hapo kwa mkopo.
“Cavani bado ana miaka mitatu mbele ya kucheza soka la kiwango cha juu na ushindani mkubwa na anataka kucheza Ulaya au Amerika Kusini, lakini itategemeana na klabu husika. Bado ana uwezo wa kucheza timu kubwa.
“Sina wasiwasi kuhusu suala la Cavani kuongezewa mkataba na PSG,” alisema wakala huyo na kuongeza.
“Usajili ujao wa kipindi cha majira ya baridi Januari, mwakani, Cavani hawezi kuondoka, ataendelea kusalia hapa.”
Tangu Cavani ajiunge na PSG, amefunga mabao 195 katika mechi 287 za mashindano tofauti. Mkataba wake unatarajia kumalizika 2020
Post a Comment