MARA baada ya kumtangaza Charles Boniface Mkwasa kukaimu nafasi ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa Yanga Mkongomani, Mwinyi Zahera, Kamati ya Ufundi ya timu hiyo imepanga kukutana kwa ajili ya kupitia mikataba ya wachezaji wake nane wa kimataifa.

Yanga, Jumanne ya wiki hii ilitangaza rasmi kuachana na Zahera kutokana na matokeo mabaya ambayo imeyapata ikiwemo kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa iliyokuwa inashiriki.

Wachezaji hao wapya ni Lamine Moro, Sadney Urikhob, Mybin Kalengo, Juma Balinya, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana, Moustafa Selemani na Farouk Shikalo.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo Championi Ijumaa imezipata ni kuwa kamati hiyo haraka itakutana kuipitia mikataba hiyo ya wachezaji wakati wakielekea kwenye usajili wa dirisha dogo linalotarajiwa kufunguliwa Desemba 16, mwaka huu.

Mtoa taarifa huyo alisema kati ya wachezaji hao wa kimataifa waliosajiliwa, wapo baadhi watakaositishiwa mikataba yao kwa kigezo cha kushindwa kufi kia malengo ili kuweza kuendana na mikakati ya Mkwasa ambaye tayari ameanza majukumu na leo ataiongoza Yanga ikicheza dhidi ya Ndanda.

Aliongeza kuwa kamati hiyo tayari imekamilisha ripoti yake na kuwajua wachezaji walioshindwa kufi kia vigezo vya kuichezea Yanga, hivyo wamepanga kuachana nao ili kuifanyia maboresho safu yao ya ushambuliaji ambayo imeonekana butu.

“Mchezo wa soka ni wa uwazi kila mtu anaona, hivyo kamati yetu ya ufundi kwa kushirikiana na kaimu kocha wetu mpya, Mkwasa ambaye ni mjumbe katika kamati hii imepanga kukutana na kupitia upya mikataba ya wachezaji wote wa kimataifa waliosajiliwa.

“Hivyo, basi tayari kamati hiyo wameshakamilisha ripoti yao mchezaji gani asitishiwe mkataba wake na yupi abakishwe kwa kuangalia idadi ya mechi za mashindano ambazo amezicheza za ligi na michuano ya kimataifa.

“Kikubwa tunataka kutengeneza kikosi kitakacholeta ushindani kwenye ligi na Kombe la FA, msimu huu na hilo linawezekana tunasubiri usajili wa dirisha dogo lifunguliwe,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela kuzungumzia hilo alisema: “Kiukweli timu yetu inahitaji maboresho makubwa kwa kusajili wachezaji wenye ubora katika usajili wa dirisha dogo. “Lipo wazi safu yetu ya ushambuliaji haipo vizuri na hilo limeonekana kwenye ligi na michuano ya kimataifa,” alisema Mwakalebela.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.