LAZIMA tuseme ukweli na siku zote ukweli unamuweka mtu huru kutokana na kuwa muwazi kwenye jambo au kitu flani.

Ukweli wangu leo ni kuhusu soka la wanawake hasa kwenye Ligi Kuu ya Wanawake inayochezwa hapa nchini kuwa tumeanza kuona matunda yake.

Ligi kuu hii imeongeza wigo wa kuzalisha wachezaji wengi wa kike tofauti na hapo awali ambapo wachezaji hawakuwa wengi kihivyo.

Wingi huo wa wachezaji kutoka kwenye klabu mbalimbali umewapa wigo mpana makocha wa timu za taifa kuchagua wachezaji kama ilivyo kwa timu za taifa za wanaume.

Kwenye michuano iliyopita ya Cecafa ya wanawake, tumeshuhudia wachezaji wengi wenye ubora ambao wote wanacheza soka hapa nchini kwenye klabu mbalimbali za hapa nchini.

Sio tu kuzalisha wachezaji, bali pia wachezaji wenye ubora na kujua umuhimu wao wakiwa dimbani.

Siku ya fainali kati ya Kilimanjaro Queens dhidi ya Kenya, nilikaa sehemu moja na kocha msaidizi wa Uganda ambaye aliniambia waziwazi kuwa kwenye michuano hiyo hakuna timu imara kama ya Tanzania Bara ambayo ni Kilimanjaro Queens.

Aliwasifu sana wachezaji wa Kilimanjaro Queens akisema wako imara na wanajua nini wanafanya wakiwa dimbani tofauti na wachezaji wa timu zingine.

Kocha huyo alienda mbali zaidi akisema angalia hata mfumo waliokuwa wakicheza wa 3-5-2 ni mfumo wa kiume tena kuna timu zingine za wanaume haziwezi kuucheza mfumo huo lakini wao wanaumudu kikweli kweli.

Wanaumudu kwa sababu ni wachezaji wenye uzoefu na wenye kutekeleza kile wanachofundishwa na walimu wao.
Sasa ukiangalia kwa kina utagundua tu kuwa klabu zetu za timu za wanawake ndio zimefanyakazi kubwa kwa sababu huko ndio wanakaa sana.

Lazima tuwapongeze waliokuja na wazo hili la kuanzisha Ligi ya Wanawake kwa sababu sasa tunashuhudia soka la kwelikweli kutoka kwao.

Najua wengi walitaka kuona tunaendelea kutetea kombe, lakini kuna wakati lazima tukubaliane na matokeo.

Kocha Bakari Shime maarufu Mchawi Mweusi, anasema amejenga timu kwa ajili ya michuano ya Afrika na sisi hilo ndio kusudio letu kubwa kuona timu yetu inafuzu kwa michuano hiyo mikubwa.

Tunastahili kushiriki michuano ya Afrika kwa sababu tuna timu imara na yenye ubora wa hali ya juu na huu ni wakati wetu na nina hakika ligi yetu ikiendelea hivi basi timu yetu ya taifa itazidi kuwa imara zaidi na zaidi.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.