LIGI kuu Bara inazidi kupamba moto na ushindani unazidi kuwa mkubwa kwa timu shiriki kutokana na ukweli kwamba kila timu inahitaji kupata matokeo chanya.
Kwenye kutafuta matokeo tumeona kwa sasa bado mwamko wa mchezaji namba kumi na mbili unazidi kuanguka siku hadi siku jambo ambalo halileti afya kwenye maendeleo ya soka.
Ni wakati muafaka wa mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kushuhudia timu zao zinapocheza jambo ambalo litaongeza morali kwa wachezaji.
Kuna baadhi ya mechi tunaona kabisa zinakosa mashabiki wa kutosha yaani wanakuwa ni wachache wa kuhesabu kabisa kwenye majukwaa yote jambo ambalo sio jema kwa timu.
Muhimu kujitokeza viwanjani kuwapa sapoti wachezaji kwani uwepo wa mashabiki ni muhimu na kunafanya wachezaji kucheza mechi za ushindani.
Mechi nyingi zinazochezwa kwa mfano nje ya mkoa wa Dar zimekuwa hazina ule mwamko mkubwa wa mashabiki licha ya timu kucheza nyumbani.
Tunaona timu kama Mbeya City ambayo inakwenda mwendo wa kusuasua imekuwa ikipata mashabiki wachache kwenye mechi zake nyingi za nyumbani hii pia huenda ni sababu kwa kiasi chake kwa timu kuboronga.
Wachezaji wanashindwa kujua iwapo wapo watu ambao wanawafuatilia hakuna anayewashangilia wala kuwazomea pale wanapochemka inaua morali kwa kiasi chake.
Kuna umuhimu mkubwa wa sapoti kwa mashabiki kujitokeza viwanjani kwani kwenye mpira kila mmoja ana umuhimu wake.
Hata timu za Dar pia hakuna timu yenye uhakika wa kupata mashabiki wengi kutokana na mwamko kuwa mdogo rai yangu kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Mchezo wa Jumatau ya wiki hii uwanja wa Taifa ambapo Yanga ilikuwa inacheza na KMC bado mashabiki hawakuwa wengi licha ya matangazo kufanyika.
Wengi wamekuwa wakikimbilia kwenye vibanda umiza hii sio tabia nzuri hasa kwa wale ambao wapo karibu na uwanja na wanaweza kufika.
Kwa wale wenye uwezo wa kufika uwanjani wanapaswa wafike ndani ya uwanja na kutoa sapoti kwa timu yao ila wale ambao wapo mbali basi itapendeza wakitazama kupitia vibanda umiza.
Kumeanza kuskika kelele kwamba waamuzi wanashindwa kufuata sheria 17 za mpira kutokana na presha kuwa kubwa ndani ya ligi pia hata kule kwenye Ligi Daraja la Kwanza.
Katika hili mamlaka husika, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa lisipuuzie malalamiko haya na kutazama kuna jambo gani ambalo linaendelea katika hili.
Tumemskia kocha wa Yanga, Boniface Mkwasa naye akizungumzia hili baada ya kupata sare ya kufungana bao 1-1 mbele ya KMC na kudai kwamba pambano liliamuliwa na mwamuzi.
Ili ligi iwe bora kila mmoja anapaswa awe makini katika kutimiza majukumu yake mwanzo mwisho ili kuendeleza ubora wa ligi yetu ambayo inafuatiliwa na watu wengi.
Ni jukumu la kila anayepewa mamlaka kufanyia kazi kwa usahihi kile ambacho anakifanya bila kumuumiza mtu, nina amini kila kitu kitashughulikiwa na mambo yatakuwa sawa.
Kwa upande wa ratiba imekuwa bado haieleweki namna inavyopangwa na kupanguliwa pia katika hili bodi ya ligi kuna umuhimu wa kulitazama hili.
Azam FC nao pia mechi yao ya hivi karibuni walilazimisha sare ya kufungana mabao 2-2 inaelezwa kuwa ratiba awali ilikuwa mechi ichezwe saa moja usiku mwisho wa siku ikabadilishwa na kupelekwa majira ya saa 10 jioni.
Suala la kubadili muda ama ratiba halikatazwi ila kikubwa ni kwamba ni wakati gani mabadiliko yanafanywa na ni nani ambaye anahusika katika mabadiliko hayo.
Dunia nzima imemshuhudia nahodha wa Azam FC, Agrey Morris akiongea kwa uchungu namna anavyoona timu yake haijatendewa haki kwa kubadilishiwa muda wa kucheza mchezo wao.
Anaeleza kuwa walipewa muda mfupi kabla ya mechi jambo ambalo limewapotezea dira na kupata sare ya kufungana mabao 2-2 wakiwa nyumbani Chamazi mbele ya JKT Tanzania.
Katika hili pia ni muhimu kuweka mpangilio mzuri kuepuka zile panga pangua za ligi ili kuona kwamba kila timu inapata muda wa kujiandaa vema na kupata matokeo ambayo wanayahitaji.
Jambo la msingi ni kuona kwamba ligi yetu inakuwa bora kuliko jana katika kile ambacho kinaendelea kwani hizi ni kazi za watu na wanategemea kupata ugali kwenye mpira.
Imani yangu ni kwamba mabadiliko yanawezekana katika hili iwapo kila mmoja hatabahatisha katika kile anachokifanya matokeo yataonekana.
Ubabaishaji muda wake kwenye soka umeisha ila kwa sasa ni lazima tukubali kwamba teknolojia imekuwa na kila kitu kipo wazi.
Jambo la msingi pia kwa wachezaji ni kutosahau majukumu yao kwa sasa kwani kuna baadhi ya timu ambazo zipo mapumziko na nyingine zinaendelea kupambana na mechi zao.
Wakati mzuri wa kujiaandaa kwa timu ambazo hazitakuwa na mechi kwa sasa na kuona namna gani zitafikia malengo ambayo wamejiwekea
Post a Comment