NOVEMBA haijawa sawa kwa baadhi ya makocha wengi hapa Bongo tumeona pia hata nje huko nako mambo yalikuwa vurugu mechi.
Tunaona kwa sasa mashabiki wa Arsenal meno nje baada ya kocha wao aliyedumu kwa muda wa miezi 18 Unai Emery kupingwa chini baada ya kupewa mikoba ya Arsene Wenger.
Huko balaa lake tuachane nalo kwa kuwa mambo yao wanayajua wenyewe na mwezi Novemba tayari umeshameguka tupo kwenye mwezi mwingine wa Desemba sasa ni muda wa kujipanga upya kujua wapi tulikosea.
Kwenye upande wetu sasa Ligi Kuu Bara ambapo bado ipo mzunguko wa kwanza tunaona kwamba makocha wengi wameachishwa kazi zao na sasa timu zitakuwa chini ya makocha wengine wasaidizi ama wale waliopewa mkataba.
Kwa sasa habari kubwa ni kocha wa Simba Patrick Aussems kusimamishwa jumla na uongozi wa Simba licha ya kuifikisha timu hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita sio tatizo kuona haya yakitokea kwa timu kubwa ni kawaida.
Sababu kubwa kila timu inayoajiri kocha inakuwa na malengo na hesabu ambazo kocha anapewa iwapo atashindwa kuzifuata basi mwisho wake unafika na maisha yanaendelea.
Ukweli ni kwamba kwa wimbi ambalo limetokea kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi hali inaonekana kuwa ni mbaya kwa makocha Bongo hapa kuna kitu ambacho kinapaswa kifanyiwe kazi.
Achana na Yanga kumfukuza Mwinyi Zahera usisahau kwamba hata Alliance FC nao walimfukuza Athuman Bilal ‘Bilo’ baada ya kusimamia mechi moja sawa na dakika tisini na alilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Mbao FC.
Kuna jambo ambalo halipo sawa kwa uongozi wa timu zetu Bongo ama ndani ya mfumo mzima wa timu zetu hasa kwenye utawala na kama huu mwanya hautazibwa mapema basi msimu huu makocha wemgi watasimamishwa kazi.
Timu zinataka matokeo huo ni ukweli tena yale mazuri lakini kuna vitu ambavyo vinachangia hayo matokeo kupatikana ndani ya uwanja na nje ya uwanja kikubwa ni kuwa na mipango thabiti na makini kwa timu kiujumla.
Matokeo yakiwa mabaya makocha wanapigwa chini hilo lipo wazi lakini wale ambao ni wahusika wakubwa wa matokeo wamekuwa wakiwaachia mzigo wa lawama makocha huu ni uonevu wa haki unapaswa upingwe kwenye timu zetu zote Bongo.
Utashangaa kwa mwendo ambao unakwenda kwa sasa hata Azam FC na Mbao pia nao watampiga chini kocha wao kwa kuwa umeshakuwa ni mtindo kwa timu zetu zikiona hakuna matokeo basi zinakimbilia kuwatimua makocha.
Msingi mkubwa wa makocha unajengwa na falsafa zao ambazo wanazisimamia pamoja na kufanya kazi kwa ushirikiano jambo ambalo linawafanya wapate matokeo chanya uwanjani.
Kuna mengi ya kufanya kabala ya kumpiga chini jumla kocha ambaye anafanya kazi na timu hasa kama amekaa muda mrefu kwa kuwa utambulisho mpya unaleta masuala mapya ambayo yanaweza kuwa magumu kwa kocha anayekuja.
Kila kocha ana mbinu zake na mipango yake anayosimamia kuifikikisha timu anapotaka je katika misingi anayopitia hakukuwa na mirija yoyote ambayo ilikuwa imekatwa na kuzuia ule mfumo wake kuwafikia walaji kwa uhakika?
Ni ngumu kuikataa hali ya makocha kutimuliwa maisha ya soka wakati mwingine yanayumbishwa na ule upepo ambao unakuwa kwenye soka wakati huo jambo la msingi kujiuliza ni maamuzi sahihi yanafanywa ama mtu mmoja tu amejiskia na kufanya mambo hayo?
Yote kwa yote makocha ambao wanapewa majukumu yao kuyasimamia nao wanapaswa wazingatie weledi wa kazi kwa kufanya kile ambacho wanakiamini kitawapa matokeo bila kugawa makundi na kugawa timu.
Tuwe wavumilivu katika mapito magumu ambayo tunapitia hasa kwetu sisi ambao tunahitaji mafanikio ya haraka hakuna kitu kama hicho kwenye soka kila kitu ni mipango na mbinu ambazo zinapangwa.
Gharama kubwa zinatumika kwa makocha kutimuliwa ambazo zingetumika kulipa masuala mengine ya msingi ambayo yanapaswa yaendelee kufanyika ndani ya timu kwa maendeleo ya taifa.
Kuna masuala ya malipo kwa wachezaji, posho na masuala mengine ya msingi ambayo yangeweza kutumia zile gharama za malipo kwa makocha wetu ambao wanafukuzwa jumla.
Tupunguze kukurupuka katika maamuzi iwapo tunaona yatatugharimu busara na hekima wakati mwingine zinapaswa zitumike kupata kile ambacho tunakihitaji licha ya kwamba tutatumia muda mrefu.
Tufanye maamuzi sahihi wakati sahihi iwapo tumekubali nakuridhishwa kwamba tunachokwenda kukifanya kipo sawa na hakuna ambaye amekurupuka katika kufanya masuala hayo ya maamuzi.
Viongozi wasifanye haraka katika kuwasimamisha na kuwafukuza makocha wanapaswa watafute suluhisho mapema kabla ya kufikia hatua ya kumfukuza kocha ambayo ni hatua ya mwisho kabisa.
Viongozi watazame vitu muhimu vya kufanya na kuwapa majukumu yanayostahili makocha ambayo wana imani kwamba watayatimiza kwa wakati bila kuboronga.
Nawaomba viongozi wawe makini katika kila hatua kwani wao ndio wanaongoza timu ambazo zinawapa furaha mashabiki suala la maumivu hakuna anayefikiria ila matokeo ya mpira huwezi kuyazuia.
Kocha anaajiliwa kwa kufukuzwa hilo lipo wazi lakini muda mwingine inapaswa kuangaliwa wakati gani anafukuzwa na amefanya nini ndani ya timu.
Iwapo vile ambavyo alifanya ni vibaya basi ni haki yake kufukuzwa na kuambiwa ukweli kwamba alikosea sehemu fulani kabla ya kuanza kumlamu kwa kushindwa kwakwe.
Kwa mambo ambayo yalikuwa kwenye mkataba kwamba iwapo atashindwa kuyafikia basi mlango wa kutoka utakuwa wazi anapaswa afungashiwe virago ila kama haikuwa sehemu ya makubaliano na masuala ya kuvunja mkataba ni wakati wa viongozi kutulia na kufanya maamzui sahihi
Post a Comment