KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ametoa angalizo kwa washambuliaji wake wote akiwemo David Molinga ‘Falcao’ na Juma Balinya kama watashindwa kubadilika kwa kuhakikisha wanafunga mabao ya kutosha katika mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, basi hawana nafasi ya kuendelea kubaki.
Zahera ametoa kauli hiyo ikiwa timu yake itaendelea kupata ushindi mdogo katika mechi zake kupitia kwa washambuliaji hao ambao mpaka sasa safu ya ushambuliaji imefunga jumla ya mabao kumi katika mechi tisa za kimashindano walizocheza.
Mbali na Molinga na Balinya, Zahera amewagusa Maybin Kalengo na Issa Bigirimana ambao kwa pamoja viwango vyao vimekuwa vya kusuasua kutokana na kuandamwa na majeraha tangu walipojiunga na Yanga.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa kama washambuliaji wake hawatabadilika kabla ya kipindi cha usajili wa dilisha dogo, hataweza tena kubaki kuendelea nao kwa kuwa watakuwa kinyume na masharti ya mikataba yao inavyosema.
“Binafsi mwenendo wa timu bado naona upo sawa, ingawa tunashindwa kupata mabao ya kutosha katika mechi zetu, najua safu ya ushambuliaji inashindwa kufunga mabao licha ya kwamba tumekuwa tukitengeneza nafasi za kuweza kufanya hivyo, kitu ambacho siyo kizuri, huwezi kuwa na washambuliaji ambao hawafungi, sasa wa nini kwenye timu?
“Watu wamekuwa wanalalamika juu ya kufunga mabao machache hata sisi kwenye benchi hilo tunaliona lakini hawajui nini ambacho kipo kwetu, wachezaji wanajua jambo gani wanatakiwa kufanya lakini kama wanashindwa nitawaondoa kwenye dirisha dogo, kwa sababu wote mikataba yao ina kipengele cha kufanya vizuri, watakaoshindwa tutawaacha, hakuna mwenye nafasi ya kudumu kati yao,” alisema Zahera.
Post a Comment