Wakati wengi wakiamini kutimuliwa kwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ni kutokana na timu hiyo kutolewa katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi Pyramids, kocha huyo amefunguka kilichopo nyuma ya pazia.

Wiki jana uongozi wa Yanga ulitangaza kuvunja mkataba na Mkongomani Zahera pamoja na benchi zima la ufundi kwa kile ilichoeleza ni kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo dimbani.

Hata hivyo, jana Zahera alianika kila kitu huku akieleza kuwa tatizo kubwa lilianzia kwa kukataa kuchaguliwa kocha msaidizi mpya, lakini akimtaja mtu mmoja kwa jina moja la Ndama kuwa alishinikiza atimuliwe.

"Uongozi ulinihakikishia hata kama tutafungwa na kutolewa na Pyramids hawatanifukuza, lakini nilishangaa (Jumanne iliyopita) wakati tupo mazoezini Meneja wa timu Hafidhi (Saleh) ananiambia naitwa klabuni na msaidizi wangu, Noel Mwandila.

"Ukweli tofauti ilianza baada ya kukataa Mkwasa asiwe msaidizi wangu, na nilikataa kwa sababu katika mkataba wangu unaonyesha msaidizi nitachagua mwenyewe."

Zahera alisema sababu nyingine ya timu hiyo kuondolewa katika mashindano ya kimataifa ni kutokana na kuwapo kwa maandalizi ya kiwango cha chini ukilinganisha na ukubwa wa mashindano hayo ya Afrika.

Kocha huyo alisema kuwa wakati wakiwa njiani kuelekea Botswana kuwakabili Township Rollers, baada ya kushuka na ndege jijini Johanesburg, Afrika Kusini, viongozi walikosa fedha ya kulipia usafiri wa basi na yeye alilazimika kutoa kiasi cha Dola za Marekani 2,000 ( zaidi ya Sh. milioni nne za Tanzania) ili kupata huduma hiyo.

"Hawakuniomba, ila wachezaji wangu waligomea kupanda basi hilo la timu pinzani, ilinishangaza, namna gani viongozi mnasafiri bila ya kuwa na fedha za dharura, na hapo Mwakalebela (Makamu Mwenyekiti- Frederick), alitangulia kuweka mambo sawa," aliongeza kocha huyo.

Alisema pia na wakati wanarejea tena Johannesburg kutoka Gaborone, wakitumia muda wa saa sita, uongozi ulisema hakuna fedha za kuwanunulia wachezaji chakula cha njiani, huku wakisema wameandaa mlo mmoja tu na baadaye wakitakiwa kusubiri usafiri kurudi nchini.

"Mwanza pia tulifikia hoteli ya maajabu, soko chini, hatuwezi kukaa hoteli hii na tunaenda kucheza mechi ya kimataifa... hoteli yenyewe wakipika chakula, wachezaji sita au saba wanakosa chakula, namshukuru bosi wa GSM, alitusaidia, tukahamia hoteli nyingine, nasema hivi ili watu wajue na wasiangalie matokeo tu," alisema Zahera.

Kocha huyo alisema pia baada ya kumaliza mechi dhidi ya Pyramids jijini Mwanza, kikosi chao kilizuiwa kuondoka hotelini mpaka watakapotakiwa kulipa deni la Sh. 545,000 na kwa mara nyingine Mwakalebela, alimweleza awasaidie kulipa na wakifika Dar es Salaam, watamrejeshea.

"Lazima wanirejeshee, kila fedha niliyokuwa natoa, tuliandikishiana na walikuwa wakirejeshe," Zahera alisema.

Hata hivyo, kocha huyo alisema kuwa Yanga haikupaswa kumtimua kwa kuangalia matokeo ya mechi dhidi ya Pyramids ya michezo minne ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo timu hiyo imecheza, ikiwa wameshinda mechi mbili, sare moja na wamepoteza mchezo mmoja.

Zahera ameitaka Yanga kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu yao na jambo hilo litasaidia kuwarejesha kwenye soka la ushindani kama walivyo TP Mazembe ya DRC au watani zao Simba.

Post a Comment

Author Name

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.