INAWEZEKANA
kabisa kuwa vile viazi vilivyokatwa katwa na kukaangwa kwenye mafuta
vinawalevya wachezaji wetu! Ndiyo hapa nazungumzia chips, chakula pendwa
cha watu wengi. Ukila zile unaonekana wa ‘mjini’ au una fedha kiasi
hata kama utakula kavu.
Ndoto za
wachezaji wengi ni kucheza soka la kulipwa, ndiyo hiyo ni dunia nzima,
kule Amerika wanawaza kwenda kucheza Ulaya hata Afrika wanawaza kwenda
huko, kwa kifupi wengi wanapenda kwenda kucheza sehemu ambayo
wataifurahia.
Sasa hapa kwetu, wachezaji wetu wengi wanapenda sana kucheza Yanga na Simba, hizi ndizo klabu kongwe na maarufu hapa Bongo.
Hata kama
zitakuwa na hali mbaya kiuchumi na wakaletewa ofa ambayo ni ndogo
tofauti na ile watakayoleta Azam au Mtibwa mchezaji hapindui kucheza kwa
kulwa na doto, hizi ndizo ndoto zao.
Anaona wazi pale
hakuna nafasi ya kucheza wala hajali atang’ang’ania hapohapo, hii yote
anataka akacheze hapo, hajali kesho yake wala kipaji chake.
Sasa wanapojiunga
na timu hizo kongwe akacheza mechi moja na kufanikiwa kuwateka
mashabiki ndiyo basi tena ataanza kwenda kujirusha na yeye.
Utamwambia nini
sasa ameshakubalika na mashabiki kwa mechi moja tu, hapo kama alikuwa
analala saa 3 usiku basi ratiba itabadilika ataanza kukesha kule
wanakopiga Wazee wa Ngwasuma, Twanga Pepeta au Sinza kwenye vibanda vya
chips.
Chips za Dar ni
tamuuu hasa Sinza na mitaa fulani sasa hapo akili yote inahama, huko
kuna vishawishi kadhaa na mchezaji asipokuwa makini basi anapotea kabisa
huyo mchezaji.
Kucheza Dar tena
Yanga au Simba na ukafanikiwa kuteka watu basi baada ya hapo inahitaji
uvumilivu na kuamini zaidi katika ndoto zako ili kuweza kukifanya kile
ambacho kimekupeleka hapo.
Tanzania tuna uhitaji mkubwa sana wa wachezaji wa kwenda kucheza nje na kuongeza uzoefu wa mechi kubwa.
Nahodha wa Taifa
Stars, Mbwana Samatta anayecheza Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji
alishasema ni vyema wachezaji wetu wengi wakatafuta nafasi ya kwenda nje
kuongeza uzoefu sasa ni wakati wenu, tumieni teknolojia iliyopo
kujiuza.
Siku hizi mambo
yamerahisishwa, unafungua akaunti yako Youtube unaomba video zao pale
Azam Media wanakupa unatupia zingine unasambaza kwenye klabu mbalimbali
duniani, sasa kama una kipaji utafanikiwa tu hata kama itakuwa kwa
kuchelewa. Yaani kama ipo ipo tuuu.
Ukishachukulia mpira kama nidyo kazi yako rasmi lazima utafuata ile misingi ya kuhakikisha unafanikiwa na kufika mbali zaidi.
Haiwezekani wewe
kila siku ukihojiwa na Waandishi wa Habari unasema unataka kwenda
kucheza soka nje ya nchi sasa mbona huendi na uwezo wa kucheza unao.
Tuliona TP
Mazembe walitua kwa Ibrahim Ajibu lakini dili likaisha juu juu tena
wakati huo kijana alikuwa moto sana, sasa nafasi kama hizi kwa nini
hamzitumii vizuri zikija. Au chips za Sinza zinawafanya mshindwe
kufikiria nje ya boksi?
Huko TP Mazembe
ndiko alikopita Samatta na amekuwa ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wa
Tanzania kutokana na uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu ndani na nje ya
uwanja jambo ambalo kimsingi limemjenga na kumfikisha hapo alipo sasa.
Safari ya
kuelekea mafanikio kama aliyokuwa nayo Samatta, inahitaji moyo wa
uvumilivu, nidhamu na kutokubali kurudi nyuma, hata kama safari hiyo ina
vigingi na miba ndani yake.
Post a Comment