KILIMANJARO Queens ipo kwenye maandalizi makali ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Afrika Mashariki ‘Cecafa’, ambayo itafanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza kuanzia Novemba 16 yaani Jumamosi ijayo.
Kilimanjaro au Kili Queens ndiye mwenyeji na pia anashikilia mataji mawili yaliyopita hivyo sasa anasaka hat trick yake ya kombe la michuano hiyo mikubwa kwa ukanda huu kwa upande wa soka la wanawake.
Michuano hii ambayo kwa mara ya kwanza ilifanyika mwaka 1986 na kufanyika Visiwani Zanzibar na wenyeji hao wakabeba uchampioni, baada ya hapo ikapita zaidi ya miaka 30 bila kufanyika.
Mwaka 2016 ikareja tena hewani, safari hii ilifanyika nchini Uganda na Kilimanjaro Queens ikafanikiwa kubeba na mwaka 2018 ikafanyika tena Rwanda hapo pia Kili ikachukua na sasa inafanyika Tanzania, kwa nini tusiweke hat trick yetu murua.
Tanzania tumejaaliwa ligi bora ya wanawake, pongeza kwa Chama cha Soka la Wanawake na Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ kwa kulisimamia hili na sasa mizizi inaonekana kushika kabisa chini.
Pia tuna kikosi bora kilichojaza wachezaji wenye vipaji vya hali ya juu, wenye kujitoa hata kama wanakuwa kwenye hali ngumu, tunafahamu Kili haina mdhamini hii ni kwa timu zote za taifa za wanawake lakini utaona namna ambavyo wanapambana kuleta mafanikio.
Sioni cha kutuzuia kuchukua ubingwa wa Cecafa kwa mara ya tatu tena kwenye ardhi yetu, kama tuliweza kubeba kwao kwa nini kwetu iwe ngumu, Cecafa moto uleule.
Ngoja nikukumbushe kwanza kabla sijafika mbali, Kili imepangwa kundi moja na ndugu zetu Zanzibar, Burundi na Sudani Kusini hili Kundi A, halafu lile B lina timu za Ethiopia, Kenya, Uganda na Djibout.
Ukiziangalia timu zote hizi hakuna wa kutuzuia kuwa machampioni jamani, Watanzania twendeni tukaujaze ule Uwanja wa Chamazi ambako ndiko michuano itafanyika, twendeni tukapate raha.
Uzuri ni kuwa wachezaji wa Kili wanafahamu Watanzania tumeshajiandaa kushangilia ubingwa hivyo sasa wanakazana kufanya mazoezi ya nguvu ili kuhakikisha hawatuangushi, binafsi nina waamini sana hawa wadada jamani.
Mechi ya kwanza ya Kili watacheza Jumamosi yaani Novemba 16, pale Chamazi sasa itakuwa aibu kama tutashindwa kwenda uwanjani kuwasapoti hawa wadada ambao wameahidi kutupatia burudani kwelikweli.
Twendeni uwanjani kwa wingi Chamazi tukajaze uwanja hadi wageni washangae na ikiwezekana wachanganyikiwe kabisa kutuona tupo majukwaani na bendera za Tanzania na jezi za timu yetu.
Unajua katika michezo wapinzani wakiona wenyeji wana mashabiki wao wengi huwa wanachanganyikiwa, hili lipo wazi na wachezaji huwa wanasema wazi kuwa wakikuta wenyeji wana wachezaji wa ziada jukwaani hupatwa na mchecheto.
Sasa hiki ningependa kuona kikitokea wakati tunacheza na Sudani Kusini hiyo Jumamosi, lazima Wasudani wakione cha moto, wachezaji wapambane uwanjani na majukwaani kuna ‘vibe’ kama loteee kutoka kwa Watanzania wapenda maendeleo kwenye michezo.
Nitakuwepo mapema kabisa Jumamosi pale Chamazi na jezi yangu ya taifa na bendera ndogo kuishangilia Kili Queens, mashabiki kujeni basi tupige stori mbili tatu huku tukipata burudani taamu kutoka kwa dada zetu ambao wamepania kwelikweli. Njooni Chamazi tuonane
Post a Comment